Mwalimu Auawa baada ya ugomvi wa picha ya Lowassa kuchanwa
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Manushi Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini ameuawa saa chache baada ya ugomvi unaohusishwa na kuchan...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/09/mwalimu-auawa-baada-ya-ugomvi-wa-picha.html
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Manushi Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini ameuawa saa chache baada ya ugomvi unaohusishwa na kuchanwa kwa picha ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Mwalimu huyo, Demetus Dastan (33) maarufu kwa jina la Kidule, aliuawa Jumamosi iliyopita usiku na mwili wake kukutwa katika shamba la mtu aliyetajwa kuwa ni Joackim Massawe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema kabla ya kuuawa, mwalimu huyo alikuwa amekwenda kunywa pombe katika klabu moja hapo kijijini. Inadaiwa kuwa akiwa klabuni, kulitokea ubishani kati yake na mtu mwingine uliotokana na kuchanwa kwa picha ya Lowassa ambao ulikwenda mbali na kusababisha wapigane.
Kamanda Ngonyani alisema waliamuliwa na wateja wengine waliokuwapo na baadaye mwalimu huyo aliondoka kurejea nyumbani na hakuonekana hadi mwili wake ulipookotwa.
Baadaye mwili wake ulikutwa shambani ukiwa na michubuko kidogo kwenye mguu wa kulia karibu na goti na shati lake likiwa limechanikachanika.
Polisi wamewakamata watu wawili akiwamo mmiliki wa klabu hiyo na mtu mwingine anayedaiwa kuwa aliongozana naye kurudi nyumbani huku mtu waliyepigana naye akiendelea kusakwa.
Lowassa aahidi makubwa Shinyanga
Wakati picha yake ikizua balaa huko Moshi, mgombea huyo anayeungwa mkono na Ukawa, aliendelea na kampeni zake mkoani Shinyanga ambako aliwaahidi wachimbaji wadogo kwamba atahakikisha wanafanya shughuli zao bila kuingiliwa na wachimbaji wakubwa wala wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Akiwa Kahama, Lowassa alisema atawaanzishia benki yao sambamba na waendesha bodaboda na mamantilie, atafanya kila njia kukamilisha mradi wa majisafi kutoka Ziwa Victoria na kufufua bandari ya nchi kavu ya Isaka.
Lowassa ambaye pia alifanya mikutano mikubwa Kishapu, Solwa na Shinyanga Mjini, alitoa ahadi hizo katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mbulu, Kahama baada ya mgombea ubunge wa Kahama Mjini (Chadema), James Lembeli kueleza matatizo yanayowakabili wananchi wa Shinyanga kwa muda mrefu.
Lowassa aliueleza umati wa wananchi waliofika hapo tangu saa tatu asubuhi kumsubiri hadi alipowasili saa 10 jioni kwa chopa akitokea Kishapu kuwa; “nashangaa sana kuhusu hii bandari ya Isaka ila nikiingia madarakani nitairejesha kwa kasi sana. Bado sijawa rais, ila kama alivyosema Lembeli, nikiingia Ikulu nitalitazama ombi lenu la kutaka Kahama kuwa mkoa.”
“Kuhusu maji, nasikitika sana kwa wakazi wa hapa kutopata maji kutoka Ziwa Victoria. Najua kero mnayoipata na nikiingia Ikulu nitakuwa na kasi ileile ili kuhakikisha kuwa mnayapata maji haya,” alisema na kushangiliwa na wananchi hao huku akisisitiza kuwa imani waliyoionyesha kwake atawajibu kwa utumishi uliotukuka.
“Naomba urais ili nilete mabadiliko katika nchi yangu, nimechoshwa na umaskini na ulegelege wa Serikali. Nitaunda serikali ambayo elimu itakuwa bure na hakutakuwa na mchango wowote.
“Nitaboresha kilimo na kuondoa ushuru. Uchimbaji mdogo wa madini nitahakikisha unabaki kwa Watanzania pekee ila wale wachimbaji wakubwa wataendelea kama kawaida,” alisema na kufafanua kuwa wawekezaji kutoka nje watapata asilimia 70 na nchi asilimia 30.”
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema katika nchi zilizotawaliwa kwa muda mrefu na chama kimoja, vyama hivyo huondolewa madarakani inapotokea viongozi waandamizi wa vyama husika wameviasi na kujiunga na upinzani kama ilivyotokea sasa.
“Mwai Kibaki alikiasi chama cha Kanu, Kenya pamoja na Profesa George Saitoti wakajiunga na upinzani, sasa ni miaka 13 baada ya Kanu kuondolewa madarakani, Kenya imeingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati.
“Lowassa amekitumia CCM katika ujana wake wote na leo ana miaka 62. Huyu (Lowassa) ndiye aliyeteuliwa aiasi CCM na kujiunga na Ukawa ili kutuongezea nguvu ya kuing’oa CCM. Wajibu wetu ni kushikamana naye kama ilivyokuwa kwa Wakenya na Kibaki na Wamalawi na Bakili Muluzi ili tuivushe nchi katika balaa la miaka 50,” alisema Lissu.