MTANZANIA ALIYEKAMATWA KWA UGAIDI KENYA: SERIKALI YATOA TAMKO
Serikali imesema inafuatilia kwa karibu maelezo yanayotolewa na Mtanzania Rashid Mberesero (20) aliyekamatwa Kenya akidaiwa kufany...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/04/mtanzania-aliyekamatwa-kwa-ugaidi-kenya.html

Serikali imesema inafuatilia kwa karibu maelezo yanayotolewa na Mtanzania Rashid Mberesero (20) aliyekamatwa Kenya akidaiwa kufanya ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa uliosababisha vifo vya watu 148.
Aidha, Serikali imewatoa hofu Watanzania na kuwaambia kuwa nchi iko salama katika suala la ugaidi. Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe jijini Dar es Salaam jana alipozungumzia mustakabali wa nchi kuelekea kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.
Chikawe alisema wizara yake inafuatilia kwa makini kile anachozungumza Mtanzania huyo katika mahojiano nchini Kenya ili kuweza kubaini kama kuna Watanzania wanaoshirikiana naye.
“Kwa sasa amefikishwa mahakamani, lakini kama serikali tunafuatilia kila anachokizungumza kwenye mahojiano na wenzetu wa Kenya ili kuweza kuwabaini kama kuna Watanzania wanaohusika ambao wapo nchini,” alisema.
Mtanzania huyo anadaiwa kukamatwa baada ya kujificha kwa saa nane akiwa amejichanganya na maiti, lakini baadaye alipanda na kujificha darini akiwa na mabomu.
Chikawe alisema tatizo la ugadi ni la kidunia, lakini aliwataarifu Watanzania kuwa nchi iko salama. “Ugaidi ni tatizo la kidunia, sehemu nyingi kuna matatizo kama hayo, napenda niwaambie Watanzania nchi yenu iko salama, tuko salama,” alisema.
Aidha, Chikawe alisema Serikali itachukua hatua kali kwa watu binafsi, vyama vya siasa na taasisi za dini zitakazobainika kuvuruga usalama na utulivu wa nchi.
Alisema uzoefu unaonesha kila ifikapo wakati wa kuelekea kufanya chaguzi mbalimbali kumekuwa kukitokea matukio yanayoashiria uvunjifu wa usalama na utulivu.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, ni vyema wananchi, vikundi zikiwemo taasisi za dini kuepuka kushiriki katika vitendo vinavyoashiria kuvuruga amani na utulivu na kuwa serikali itachukua hatua za kisheria kudhibiti hali hiyo.
“Kazi ya serikali ni kuhakikisha kuwa usalama wa watu wote unaimarishwa ili shughuli zote zikiwa ni za kisiasa, kidini, kijamii na kiuchumi zinatekelezwa kwa misingi ya kisheria,” alisema.
Chikawe ameonya viongozi wa taasisi za dini kutoendelea kutoa matamko yanayoashiria kuingilia masuala ya kisiasa kinyume na sheria ya vyama na katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
Alitolea mfano tamko lililotolewa na viongozi wa taasisi za dini wakilenga kuwashawishi waumini wao wafuate maelekezo yao kuhusiana na masuala ya Katiba Inayopendekezwa na kuhusu uchaguzi mkuu ujao.
Alisema viongozi wa taasisi za dini wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi ila ni kinyume cha sheria kutumia uongozi wao kushawishi waumini wao watekeleze matakwa yao ya kisiasa.
“Mfano mwingine ni pale kiongozi au viongozi wa dini wanapochangisha fedha na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Hii si kazi ya taasisi za dini na ni kinyume cha sheria,” alisisitiza.
-HABARILEO