BABA WA MTOTO ALBINO, WAGANGA 10 WATIWA MBARONI
Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu 17 wakiwemo waganga wa jadi 10 wakihusishwa na tukio la kikatili katika...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/03/baba-wa-mtoto-albino-waganga-10-watiwa.html
Polisi
mkoani Rukwa inawashikilia watu 17 wakiwemo waganga wa jadi 10 wakihusishwa na
tukio la kikatili katika kijijini cha
Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ambako mtoto mlemavu wa ngozi (albino), Baraka Cosmas mwenye umri wa miaka 6 (pichani) mwishoni
mwa wiki alishambuliwa na kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu
wasiojulikana.
Miongoni
mwa watuhumiwa waliokamatwa ni watu saba ambao wanatuhumiwa kushiriki katika
kumkata kiganja mtoto huyo mlemavu wa ngozi akiwemo baba yake, mzazi Cosmas
Yoram (32).
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Ferdinand Rwegasira amethibitisha kukamatwa
kwa watuhumiwa hao kufuatia
msako mkali uliofanyika katika vijiji
vinne vya wilaya za Sumbawanga na Nkasi.
Aliwataja
waliokamatwa pamoja na baba mzazi wa
mtoto huyo kuwa ni pamoja na Mwendesha William (30),
Masunga Bakari (50), na Ngolo Masingija (47) wote kutoka kijiji cha Kaoze .
Wengine
ni Paschal Jason (40), David Kiyenze (45) na Mageta Shimba (46), wote wakazi
wa kikiji cha Kipeta , Bonde la Ziwa
Rukwa wilayani Sumbawanga.
Kwa
mujibu wa Rwegasira, katika msako huo
pia walikamatwa waganga wapiga
ramli chonganishi 10 akiwemo Sererino Kachingwe “Nakalango”(70), mkazi wa
kijiji cha Miangalua wilayani
humo ambaye pia alipatikana na bunduki aina ya Shot gun greener
yenye namba G 73354 TZD,CAR 47478
ambayo anaimiliki isivyo halali .
“Mtuhumiwa
huyu pia ni mganga wa kienyeji ambapo
alikutwa na wanyama wawili aina
ya Kalunguyeye wakiwa hai pamoja na dawa mbalimbali za miti shamba. Pia katika msako huo amekamatwa mganga mwingine wa kienyeji ,
Eliza Malongo mwenye umri wa miaka 36
mkazi wa kijiji cha Kamnyalila akiwa na
nyara za Serikali, “ alieleza.
Aliongeza
Eliza alikutwa na ngozi ya chui, wanyama wanne waliokaushwa aina ya Kalunguyeye
na nywele zinazodhaniwa kuwa za binadamu pamoja na mfupa wa swala.
Waganga
wengine waliokamatwa katika msako huo ni pamoja na Sodeli Malimbo ‘Chuchi” (69)
mkazi wa kijiji cha Miangalua, Akobo Chinzwe (50), Leonard Samson (59) na
Engelbert Kasinde (45) , wote wakazi wa kijiji cha Kamyalila.
Katika
orodha hiyo wapo Boniface Chalya
(49) na Julius Simbamwene (40) wote
wakiwa wakazi wa kijiji cha Mpui .
“Watuhumiwa
hawa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kupigia ramli vikiwemo
vioo viwili, pembe moja, ndege na
wanyama ambao hawakuweza kutambulika mara moja, mizizi ya
aina mbalimbali na dawa mbalimbali za kienyeji,“ alieleza Rwegasira.
Akifafanua
zaidi, Rwegasira alidai kuwa msako huo pia ulifanyika wilayani Nkasi
ambako alitiwa nguvuni mganga wa kienyeji
aitwae Charles Misalaba (47) , mkazi wa kijiji cha Kacheche ambapo
alikutwa na yai la mbuni , kucha
za chui , pembe ya korongo , ngozi ya paka pori
na kobe aliyekaushwa.
Amesisitiza
kuwa msako huo bado unaendelea na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara tu baada ya upelelezi wa awali wa shauri
lao kukamilika
Kwa
mujibu wake msako huo unafuatia watu wasiojulikana kumshambulia
na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na
kisha kutokomea nacho kusikojulikana usiku wa kuamkia Machi 08, mwaka huu.
Tukio
hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani
Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na
Prisca Shaaban pamoja na watoto wengine wawili ambao nao
ni albino wakiwa na umri wa miaka
nane na minne.
Alisema
tukio hilo ni la saa nane usiku wa
kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto
huyo hakuwepo wakati huo.
Akielezea
zaidi, Kaimu Kamanda Rwegasira alisema
usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na
mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na
kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia
mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
“Baada
ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka
kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa
kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya …
“Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika
hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na
kuondoka nacho kusikojulikana,” alibainisha.
Aliongeza
kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala
katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kwa
mujibu wa Rwegasira , mtoto huyo na mama yake
walikimbizwa katika Kituo cha
Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya ambapo walipewa huduma ya kwanza kisha
wakahamishiwa Hospitali ya wilaya ya Mbozi ambapo
baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya kwa matibabu
zaidi.