Uandikishaji daftari la wapiga kura bado
Tume ya uchaguzi nchini Tanzania imesogeza mbele kwa wiki moja zaidi tarehe ya kuzinduliwa kwa zoezi la daftari la wapiga kura litakalo...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/02/uandikishaji-daftari-la-wapiga-kura-bado.html
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuvipa fursa vyama vya kisiasa kujiandaa na kuandaa watu wake. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa wamesema kauli hiyo haina ukweli wowote na kwamba tume inajikosha kwa sababu haina vifaa vya kutosha vya kuendesha uandikishaji huo. Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau kutoka Dar es Salaam ametuandalia taarifa ifuatayo:
Wakati ikiwa imesalia miezi miwili tu na wiki kadhaa kabla ya tarehe iliyopangwa ya kupiga kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, wasi wasi unazidi kutanda miongoni mwa viongozi mbali mbali wa vyama vya kisiasa hapa nchini Tanzania, iwapo Tume ya Uchaguzi nchini humu itaweza kuboresha daftari la wapiga kura katika kipindi cha muda mfupi uliobakia. Baadhi ya viongozi hao wamesema kwamba licha ya tume hiyo kutovishirikisha vyama vya kisiasa katika baadhi ya maamuzi yake, lakini pia wamebaini kwamba mpaka sasa tume hiyo inakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya uandikishaji kwa sababu havijaingia nchini kama ambavyo anabaini Freeman Mbowe mwenyekiti wa Chadema.
Hata hivyo, Jaji Damian Lubuva ambaye ndiye mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania anasema madai hayo ni uoga wa wanasiasa ambao hawataki mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi.
Uandikishaji wapigakura umepangwa kufanyika nchi nzima kwa muda wa siku sitini kuanzia mkoani Njombe tarehe 23 mwezi huu ambapo watanzania zaidi ya milioni 23 wanatarajiwa kujitokeza katika uandikishaji huo. Hata hivyo kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, haijafahamika iwapo raia wengi watajitokeza kwa sababu kazi ya kuwahamasisha raia bado haijafanyika na vile vile baadhi ya watanzania wanaweza kuikosa fursa hiyo ikizingatiwa ni msimu wa wakulima kuingia mashambani kabla ya mvua za masika. Aboubakar Famau, Dira ya Dunia, BBC, Dar es Salaam.