Mkuu wa Wilaya,Wakurugenzi wapandishwa kizimbani kwa Rushwa
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu. Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, ...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/02/mkuu-wa-wilayawakurugenzi-wapandishwa.html
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu na wakurugenzi wawili wamepandishwa kizimbani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa makosa mawili yanayohusiana na rushwa.
Aidha, kesi hiyo inawaunganisha maofisa wengine wawili wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi ambapo wanatuhumiwa kuisababishia halmashauri hasara ya Sh milioni 3. Kesi hiyo iliyopewa jina la kesi ya uhujumu uchumi namba moja ya mwaka 2015, ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi.
Kwa mujibu wa, Mwendesha mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Imani Mizizi alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari 2011 watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la rushwa kinyume na kifungu cha 32 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Kosa la pili linalowakabili watuhumiwa watatu katika kesi hiyo, ambao ni Shimwela ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara/Mikindani, Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo na Cosmas ambaye ni fundi ujenzi, ni lile la matumizi mabaya ya ofisi kinyume na kifungu cha 31 cha sheria kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Watuhumiwa wengine katika shitaka hilo ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mikindani mkoani Mtwara, Limbakisye Shimwela ambaye wakati kosa hilo likitendeka kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, alikuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi na mwingine ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Biharamulo mkoani Kagera, Nasibu Bakari
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, watuhumiwa hao watatu walitumia ofisi vibaya kwa kuingia mkataba na Fedrick Zaveri kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, bafu za kuogea na mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Ihalimba bila kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.
