WAZIRI MKUU AMPA DED UYUI SIKU 60 KUHAMA NA TIMU YAKE
https://samchardtz.blogspot.com/2014/10/waziri-mkuu-ampa-ded-uyui-siku-60.html
………………………………………………….
*Asema lazima wajali matatizo ya wananchi, wasijifanye wakubwa mno
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amempa miezi miwili Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, Bi Khadija Makuani kuhakikisha kuwa
watumishi wote wa wilaya hiyo wanahamia Isikizya yalipo makao makuu ya
wilaya hiyo.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 11, 2014) wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa Isikizya waliofika kushuhudia uzinduzi wa makao
makuu ya polisi ya wilaya hiyo.
“DED
nimekagua nyumba ya mkuu wa Wilaya na kuzindua nyumba zile nane,
miundombinu iliyopo inatosha, hamia wewe na watu wako. Ninataka ifikapo
Desemba 31, mwaka huu wote muwe Isikizya. Atakayegoma, RC niletee jina
lake,” amesema Waziri Mkuu.
“Shauku
ya wananchi kuwasubiri mhamie hapa imetosha. Mtumishi ambaye atagoma ni
ishara kuwa hataki kuwahudumia wananchi, na sisi tutasema hatukutaki.
Tatizo la watumishi wengi ni kujifanya wakubwa mno kuliko wananchi
mnaowahudumia,” alisema huku akishangiliwa na wakazi wa Isikizya.
Waziri
Mkuu ambaye aliwasili mjini Tabora jana mchana, alitembelea makao makuu
ya wilaya hiyo ili kukagua mradi wa ujenzi wa makazi ya watumishi wa
wilaya hiyo. Mara baada ya kuwasili wilayani humo, Waziri Mkuu alizindua
nyumba nane za watumishi zilizojengwa kwa gharama ya sh. milioni 555
ambazo kati yake, sh. milioni 400 ni ruzuku kutoka Serikalini
Pia
alikagua ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui ambayo iko katika
hatua za mwisho za ujenzi. Kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Waziri
Mkuu alikagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja la ofisi ya Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ambalo awamu ya kwanza ya ujenzi itagharimu sh.
bilioni 1.1/- na awamu ya pili itagharimu sh. bilioni 1.4/-.
Alisema
wakati wakisubiri ujenziwa ofisi yao ikamilike, watafute nafasi kwenye
ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili waweze kuwa karibu na wananchi na
kuwahudumia kutatua changamoto zinazowakabili.
“Mnakaa
Tabora mjini halafu mnadai mnawatumikia wnanchi wa Uyui. Haiwezekani
kabisa. Hayo mafuta mnayotumia kwenda na kurudi mjini si mngetembelea
wananchi wa vijijini na kuhimiza shughuli za maendeleo?” alihoji.
“Hamieni
hapa muweze kutatua changamoto za wananchi. Kama mngehamia mapema hata
tatizo la maji lingekwishatatuliwa na ujenzi wa nyumba za watumishi wote
ungeshakamilika.”
Kuhusu
changamoto ya uhaba wa maji, Waziri Mkuu aliahidi kuwatafutia sh.
milioni 200/- kutoka wizara husika ili ziwezeshe kuvuta maji kutoka
chanzo cha Igombe kilichopo km. 35 kutoka Isikizya
Aliwapongeza
askari ambao wameamua kuhamia katika wilaya hiyo na kuishi Isikizya
licha ya mazingira magumu waliyoyakuta. Alisema atawasiliana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini (IGP) ili waone namba ya kuwasaidia kuapata walau
nyumba pacha mbili au tatu (two in one) zinazojengwa na Shirika la
Nyumba la Taifa wilayani humo.
Alimtaka
pia Mkuu wa Mkoa huo, Bibi Fatma Mwassa aangalie uwezekano wa kuwatumia
vijana waliojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kupata utaalamu
wao na kuuhamishia kwa wananchi. “RC tafuteni namna ya kutumia utaalamu
wa hawa vijana wa JKT ili wawafundishe wananchi mbinu za kilimo bora,
ufugaji bora ama ujenzi wa nyumba bora. Siyo mnawatumia kwa kuimba tu,”
alifafanua.