Kizungumkuti:Utata Kura za Wajumbe wa Bunge la Katiba Waliokwenda Hijja
https://samchardtz.blogspot.com/2014/10/kizungumkutiutata-kura-za-wajumbe-wa.html?m=0
.jpg)
Utata umezidi kugubika kura mbili zilizowezesha kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa ambayo wiki iliyopita ilikabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini Dodoma.
Utata
huo unatokana na kura za wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
upande wa visiwani, wajumbe waliokuwa Hijja, Saudi Arabia na zile za
baadhi ya wajumbe wanaodaiwa kuhamishwa kinyemela kutoka Bara kwenda
Zanzibar au kinyume chake.
Utata Saudia
Chanzo
chetu kutoka Dodoma kilisema: “Kuna utata maana hakuna uhakika iwapo
kweli mahujaji ambao ni wajumbe wa Bunge la Katiba walipiga kura maana
kuna barua ilitoka ubalozini Saudi Arabia ikisema hilo lisingewezekana.”
Uchunguzi
wa gazeti hili umebaini kuwa Ubalozi wa Tanzania Riyadh, uliandika
barua kwa Bunge Maalumu la Katiba ukieleza kwamba usingeweza kuratibu
upigaji kura kutokana na mazingira halisi ya ibada ya Hijja.
Miongoni
mwa sababu zilizotolewa na ofisi ya ubalozi huo ni kwamba mtu yeyote
ambaye si hujaji hakuwa anaruhusiwa kuingia katika maeneo ya Hijja na
Serikali ya Saudi Arabia ilikuwa imetoa vitambulisho maalumu kwa
mahujaji tu.
Katibu
wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alikiri kupokea barua kutoka
Ubalozi wa Tanzania uliopo Riyadh, ukieleza kwamba mazingira
yasingeruhusu wajumbe hao wanane kupiga kura, lakini akasema walitumia
njia nyingine kufanikisha kazi hiyo.
“Tulipokea
barua hiyo kweli na pengine niseme tu siyo moja, zilikuwa barua kama
tatu au nne hivi, maana hata hapa foreign (Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa) Dar es Salaam walituandikia kuhusu ugumu
wanaouona, lakini baada ya kuona hivyo tuliamua kutumia njia zetu
wenyewe.
“Tulimtuma
ofisa wetu kwenda Saudi Arabia na tulimkatia tiketi na kusema kweli
wakati wote alikuwa akiwasiliana nasi, nakumbuka mtu wa kwanza kupiga
kura alikuwa Raza (Mohamed, Mwakilishi wa Uzini) ambaye alikuwa Dubai na
baada ya hapo alikwenda walikokuwa mahujaji wengine na walifanikisha
vizuri sana,” alisema.
Wajumbe
wengine waliokuwa Uarabuni kwa mujibu wa orodha iliyotangazwa na
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta ni pamoja na Dk Abdallah
Kigoda, Sheikh Mussa Kundecha, Hamza Mustapha Njozi, Dk Maua Daftari,
Shawana Bukheti Hassan, Asha Mtwangi, Amina Andrew Clement na Riziki
Lulida.