mh! Mbowe, polisi uso kwa uso
https://samchardtz.blogspot.com/2014/09/mh-mbowe-polisi-uso-kwa-uso.html
Jopo la Wanasheria wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), pamoja na wanachama wake, wanatarajia
kuunganisha nguvu leo kumsindikiza Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe,
kuelekea Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya mahojiano na maofisa wa
jeshi hilo.
Jeshi hilo limemuita Mbowe, lakini chama
chake kinasema hakielewi kiongozi huyo anaitwa kwa sababu
zipi.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Willibroad Slaa, alisema Mbowe atakwenda
polisi leo kwa lengo la kuitika wito wa jeshi hilo.Dk. Slaa, alisema
uamuzi wa Mbowe kuitikia wito wa kwenda kuhojiwa na jeshi hilo
ulitokana na Kamati Kuu iliyokaa juzi licha
ya kwamba barua ya wito huo haielezi sababu za kuitwa kwake.Naibu
Katibu Mkuu Bara ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema
wameweka nguvu kubwa ya wanasheria watakaomsindikiza mwenyekiti wao
wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.Aliwataja
wengine ambao wamethibitisha kuungana na Lissu kuwa ni Mabere Marando
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Abdallah Safari, Peter
Kibatara na wanasheria wengine wa chama hicho ambao hawakutajwa
majina.Alisema mbali na wanasheria wa chama, lakini pia wanasheria
wengine wanaweza kuongezeka kwa kuwa wametoa wito kwa wanasheria wengine
watakaopata nafasi ya kuungana na hao.Akizungumzia suala hilo, Lissu
alisema yeye kama Mwanasheria Mkuu wa chama hakukubaliana na wito wa
jeshi hilo kwa kuwa barua haikuwa inaeleza sababu za Mbowe kuitwa na
kuhojiwa, lakini baada ya Kamati Kuu kukaa waliamua aende.
“Barua ya Jeshi la polisi ilitakiwa
kueleza sababu ya wito, ushauri wangu kama mwanasheria nilikuwa nimesema
asiende, lakini kwa sababu tulijua jeshi letu halifuati sheria na mara
nyingi hutumia nguvu, Kamati Kuu ikashauri kwamba aende,” alisema Lissu.
Aidha, Dk. Slaa, alisema kuwa
wanaamini kwamba wito wa kuitwa Mbowe umetokana na shinikizo la Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro alilotamka wazi bungeni
Jumatatu wiki hii usiku na kusema atahakikisha maandamano yaliyotangazwa
na Chadema ya kupinga Bunge Maalum la Katiba hayafanyiki.
Alisema msimamo wa kufanya maandamano
bado upo pale pale na kwamba tayari baadhi ya vikundi katika ngazi
mbalimbali vimeanza kuwasilisha ripoti ya maandalizi ya maandamano hayo
na pindi yakikamilika wataeleza kwa vyombo vya habari siku rasmi ya
kuanza.
Dk. Slaa alisema maandamano
yaliyotangazwa na Chadema ni ya amani ambayo Jeshi la Polisi
halikutakiwa kuyazuia isipokuwa lingetakiwa kufahamu yanaanza lini ili
kuimarisha ulinzi kama sheria inavyoeleza.
Alisema chama chochote cha siasa chenye usajili kina haki ya kufanya maandamano bila kuzuiliwa na mtu yeyote.
KAULI YA POLISI
Wakati chama hicho kikimruhusu Mbowe
kwenda kuhojiwa, Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa mpango wa kumhoji
kiongozi huyo upo palepale.
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai, Hezron Gimbi, alisema jana siku ya Mbowe kuhojiwa
anayeijua ni Issay Mngulu, ambaye amekuwa akiwasiliana na kiongozi huyo.
Akijibu maswali ya waandishi wa
habari juu ya kumtaka Rais kusimamisha Bunge Maalum la Katiba, Dk. Slaa,
alisema maamuzi hayo hayakuwa ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) pekee kama baadhi ya wajumbe wa kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) wanavyozungumza katika vyombo vya habari, bali yalikuwa
ni maamuzi ya vyama vyote vilivyoshirikishwa na TCD kikiwamo Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Aidha, Dk. Slaa, alisema kati ya
mambo ambayo Kamati Kuu iliazimia katika kikao chake cha juzi ni pamoja
na kushirikiana na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya CUF na
NCCR-Mageuzi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika
Desemba mwaka huu ili kuhakikisha wanashinda viti pamoja na uchaguzi
mkuu wa mwakani.
Suala lingine ni kuendelea na msimamo
wa kufanya maandamano nchi nzima wa kuwashawishi wananchi wasipige kura
ya kuikubali Katiba mpya, ikiwa Bunge hilo litaendelea kung`ang`ania na
uchakachuaji wa Rasimu ya katiba hiyo.
Akifafanua kuhusiana na madai kwamba
wajumbe wa Ukawa walitoka katika Bunge la Katiba wakiwa wamesaini fedha
za vikao, Lissu alikanusha na kusema kwamba mwisho wao kusaini fedha
ilikuwa Aprili 14 na Aprili 16 walitoka bungeni.
MAANDAMANO DODOMA YAFUTWA
Katika hatua nyingine, Jeshi la
Polisi mkoani Dodoma limezuia maandamano ya Chadema kwa maelezo kuwa
yanapinga Bunge Maalum la Katiba ambalo lipo kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza jana na waandishi wa
habari mjini hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel
Lukula, alisema wamepokea taarifa kutoka kwa chama hicho kikitaka
kufanya maandamano kuanzia viwanja vya Mwalimu Nyerere hadi bungeni.
Alisema pia taarifa hiyo imeeleza
kusudio la kufanya maandamano ya amani katika wilaya zote za mkoa huo
leo kupinga mchakato wa Bunge hilo unaoendelea mjini hapa.
“Jeshi la Polisi linalinda sheria
zilizopo na mtu anayepinga Bunge la Katiba kwa sasa ni uvunjifu wa
sheria kama anataka aende mahakamani,pia nawaomba wananchi msiende
kushiriki katika maandamano kwani ni batili na yanafanyika siku ya
kazi,” alisema Lukula.
Alisema alifanya mazungumzo na
viongozi mbalimbali wa Chadema kwa zaidi ya saa mbili, lakini
hawakubaliana kutokana na viongozi hao kusisitiza kuandamana leo.