HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. MCH. PETER SIMON MSIGWA, (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/hotuba-ya-msemaji-mkuu-wa-kambi-rasmi.html
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Frank Herbert aliwahi kusema
“Utawala
bora, kamwe hautegemei Sheria bali sifa binafsi za wale wanaotawala.
Vyombo vya Serikali mara zote vipo chini ya wale wanaowaongoza. Kwa hiyo
sifa muhimu ya Serikali ni namna ya kuteua/kuchagua viongozi”Serikali
ya awamu ya nne, imeshindwa kuwajenga viongozi wake katika misingi bora
na ndio maana pamoja na matatizo ya kimfumo, wizara ya Maliasili na
Utalii imeendelea kubadilisha viongozi na matokeo ya ufanisi wake
yamekua ni kioja na dhihaka katika utendaji.
2.0 UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO 16 YA BUNGE
Mheshimiwa
Spika, kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
ilileta Bungeni taarifa yake tarehe 20 Disemba 2013 liyowasilishwa na
Mwenyekiti wake, Mhe. James Lembeli kuhusu uchunguzi wa matatizo katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyokua na maazimio kumi
na sita (16). Taarifa hiyo ndiyo iliyomuondoa aliyekua Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na mawaziri wengine.
Mheshimiwa
Spika, mojawapo ya maazimio ya Bunge, yaliyoongezwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ni pamoja kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama.
Aidha, ni takribani miezi zaidi ya mitano kupita tangu Serikali iahidi
Desemba mwaka jana, kuahidi, kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kuunda tume maalumu ya kuchunguza kilichotokea wakati wa
Operesheni Tokomeza Ujangili. Katika makujukumu yake, Tume hiyo imepewa
kazi zifuatazo;
a) Kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa;
b) Kuchunguza na kubaini iwapo sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza operesheni hiyo.
c) Kuchunguza na kubaini kama kuna mtu aliyekiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea wakati wa operesheni;
d)
Kuchunguza na kubaini kama kuna watu ambao walikiuka sheria yoyote
wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo na kupima kama hatua
zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki;
e)
Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu ambaye
itabainika alikiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea pamoja na
kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza
operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na kuundwa kwa Tume hii lakini Serikali haikupaswa tena
kuipa tume kazi mpya katika maeneo yote bali yale
yaliyohitaji ushahidi wa ziada wa kijinai, hii ni kwa sababu makosa
mengine yako wazi ambayo Serikali ilipaswa iwe imeshachukua hatua badala
ya kusingizia inasubiri taarifa ya tume. Kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni, sasa inaitaka Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa
maazimio ya Bunge wakati wa Majumuisho ya Bajeti ya Wizara ili maazimio
ya Bunge hili yasiishie kabatini kama ilivyokuwa kwa mengine ya miaka ya
nyuma na ilivyozoeleka sasa.
2.1 Uwajibishwaji Wa Watendaji Kutokana Na Maazimio Ya Bunge
Mheshimiwa
Spika, aidha katika azimio namba Saba (7), Bunge liliazimia pia
kumwajibisha Mkurugenzi wa Wanyamapori Prof. Alexander Songorwa kwa
kutoa taarifa zisizo sahihi kwenye vyombo vya habari na kuudanganya umma
kuhusu mazingira na kifo cha Emiliana Marrow wa Babati.
Mheshimiwa
Spika, katika hali ya kushangaza Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa,
Mhe. Lazaro Nyalandu ambaye akiwa katika nafasi yake ya unaibu waziri,
kipindi kifupi tu kabla ya uteuzi wake, kwa kasi ya ajabu aliandaa
mikutano mingi na ziara mbalimbali huku akiandamana na lundo la vyombo
vya habari kama kumbikumbi,na kutoa matamko makali dhidi ya ujangili na
watumishi wasio waaminifu. Akiwa katika ziara hizo, aliwahi kuikandia
sana Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili iliyoongozwa na
Mhe. James Lembeli, huku akidai kuwa ilikuwa ya uwongo mtupu. Lakini
baada ya kubanwa zaidi, alikana kutoa kauli za kuikosoa ripoti hiyo ya
kamati. Sababu za kwanini akanushe maneno aliyoyasema zaidi ya mara nne,
inabakia kuwa siri yake mwenyewe.
Mheshimiwa
Spika, Waziri Nyalandu alitoa taarifa za kuwavua nyadhifa zao
Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya
Matumizi Endelevu ya Wanyamapori nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa moja
ya sababu za kuwaondoa, ni kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli
kutokana na kutowajibika wakati wa Operesheni Tokomeza. Jambo la
kujiuliza, kama aliwahi kusema kuwa taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je
ni lini amethibitisha kuwa kile alichodai kwamba ni uwongo, ulikuwa
ukweli? Cha ajabu, aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul
Sarakikya aliyekuwa kiongozi wa utekelezaji wa operesheni tokomeza na
aliyehusika moja kwa moja na kinachodaiwa kuwa uvunjifu wa haki za
binadamu, ndiye amepewa nafasi ya kukaimu ukurugenzi! Wote tunafahamu
ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukatili uliofanywa katika
operesheni tokomeza kiasi cha kusababisha mawaziri wanne kuwajibishwa
kwa kutenguliwa nafasi zao.
Mheshimiwa
Spika, aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza
ilitumia vigezo gani kumteua Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa
Wanyamapori huku ikijua alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na
jinsi aliyoendesha operesheni tokomeza ujangili iliyokuwa imejaa
dhuluma, uporaji, utesaji na udhalilishaji dhini ya wananchi. Jambo
ambalo liliishangaza zaidi Kambi Rasmi ya Upinzani ni kitendo cha Waziri
Nyalandu kumteua Ndugu Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa
Wanyamapori huku akijua kuwa Sarakikya alifanya makosa mengi katika
utendaji wake wa kazi katika idara hiyo ya Wanyamapori.
Mheshimiwa
Spika, ikumbukwe pia kuwa Ndg. Sarakikya ndiye aliyeongoza kikosi cha
kuzuia ujangili hata kabla ya operesheni tokomeza. Katika kipindi hicho,
Tanzania ilishika nafasi ya kwanza kati ya nchi nane duniani
zilizoongoza kwa matukio ya ujangili. Aidha, ili kuonyesha kwamba
Serikali hii haizingatii weledi katika utendaji, alietuliwa tena
kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili.
2.2 Kauli Tata Za Serikali Juu ya Kufukuzwa Kazi kwa Wakurugenzi
Mheshimiwa
Spika, mara baada ya waziri kutangaza kuwavua nyadhifa zao wakurugenzi
hao tarehe 24 Februari 2014, Katibu Mkuu wa wizara hii Bi. Maimuna
Tarishi aliwarudisha kazini wakurugenzi hao huku Serikali nayo kwa
kupitia kurugenzi ya habari maelezo,ikitoa taarifa kwa vyombo vya habari
kuwa taarifa za kufukuzwa kwa wakurugenzi hao si sahihi. Pia, Ikulu kwa
kupitia Katibu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, ilitoa tamko la kuitaka
Wizara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma za
kumfukuza mtumishi kazi.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Kifungu cha
IV (23) (2) inayozungumzia mamlaka ya Rais kumwondoa mtumishi
aliyemteua kazini, amri ya kumfukuza mtumishi wa umma itatekelezwa
iwapo;
(a)hati ya mashtaka imeandikwa dhidi yake (b)mtumishi wa umma amepewa nafasi ya kujibu mashtaka hayo
(c)Maombi yametolewa kwenye hati ya mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizo chini ya kifungu namba 34.
Swali
la kumuuliza Waziri Nyalandu, je, hatua hizi zilifuatwa katika
kuwasimamisha kazi wakurugenzi hawa? Na je, maamuzi yake ya kumfukuza
Prof. Songoro katika vikao vya kamati na kumdhalilisha hata baada ya
Ikulu kutoa maagizo ya Wizara kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za
kufukuza watumishi kazi ni utawala bora?
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali na Wizara
kuhakikisha kuwa, uamuzi wowote uliofanywa na kuendelea kufanywa katika
kutekeleza maazimio ya Bunge katika kuwawajibisha watumishi hao
uzingatie sheria, taratibu na kanuni kwa kuwa Sheria na Kanuni hizo
zinaeleza wazi hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Vilevile, tunasikitishwa
na mvutano baina ya waziri na katibu mkuu wa wizara, hali ambayo
inaonesha kuwa kuna mgongano aidha wa kimaslahi na hivyo kuthibitisha
kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, Waziri na Katibu Mkuu wa wizara moja
wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja akionekana kumvizia
mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya
Bunge lako tukufu.
Aidha,
mvutano huu pia ni ishara kuwa, maazimio ya Bunge yanaendelea kupuuzwa
na Serikali kwa kigezo cha kuzingatia sheria na kanuni huku zikiwaacha
watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo na idara na kuendelezea
urasimu uleule hata uko wanapohamishwa.
Mheshimiwa
Spika, ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi
mnafiki na debe tupu haliachi kutika (si maneno yangu, bali ya wahenga).
Si mara ya kwanza, kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya usafi wa
Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii, na mara kadhaa
tumeonesha kwa kiasi kikubwa udhaifu wake na kutoa vielelezo mbalimbali
vinavyotilia shaka utendaji wake kabla na hata baada ya kukabidhiwa
wizara hii nyeti!
3.0 TASWIRA YA TAIFA KATIKA JUMUIA ZA KIMATAIFA
Mheshimiwa
Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani imeendelea kutoa taarifa
kwa Serikali juu ya mtandao wa kimataifa wa ujangili ambao pia
unahusisha viongozi waandamizi wa Serikali, maafisa usalama wa taifa,
wanajeshi wafanyabiashara wakubwa, polisi, wanasiasa, Ikulu na watumishi
wa umma. Serikali ya CCM imekua ikitoa kauli za kubeza pamoja na majibu
mepesi ya tuhuma hizi huku tatizo la ujangili likiendelea kulichafua
taifa katika jumuia ya kimataifa.
Mheshimiwa
Spika, katika hali ya kushangaza baada ya gazeti la Mail on Sunday la
nchini Uingereza kutoa taarifa kuwa biashara ya ujangili inahusisha watu
wa karibu na Rais wakiwemo wanasiasa, maafisa wa Serikali na wafanya
biashara wakubwa, Serikali ilitoa matamko mbalimbali pamoja na kulaani
taarifa ya gazeti hilo na hatimaye Waziri Nyalandu, alimwalika mwandishi
wa gazeti hilo kujionea mwenyewe shughuli za Serikali za kupambana na
ujangili ikiwemo kutembembelea ghala ya kuhifadhia pembe za ndovu
zilizokamatwa. Mwaliko huo ilikua ni katika kuthibitisha kuwa Serikali
ya CCM haina la kuficha.
Lakini
katika hali ya kushangaza, uchunguzi na taarifa zaidi umeonesha kuwa
ndani ya miaka minane (8) Serikali ya CCM, imekua ikiomba kibali bila
mafanikio kutoka CITES (Convention on International Trade on Endangered
Species) cha kuuza shehena ya pembe za ndovu takribani 34,000 zenye
uzito wa tani 125 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 150 sawa
na shilingi Bilioni 244.5 za kitanzania (kwa wastani wa sh.1630 kwa dola
1).
Mheshimiwa
Spika, jumuia ya kimataifa imeshangazwa na kitendo cha Tanzania kuomba
kibali cha kuuza shehena iliyokamatwa ya pembe za ndovu kwa kuwa ni
biashara haramu na kitendo cha Serikali kuomba kuyauza ni sawa na
kuchochea ujangili zaidi kwa kuwa hali hii itaongeza uhitaji wa pembe za
ndovu kwenye soko haramu nchini China. Jambo hili ni aibu kubwa kwa
taifa kuomba kufanya biashara haramu kwa kuwa imelidhalilisha taifa. Hii
ni sawa na Serikali ikamate madawa ya kulevya, halafu iamue kuyauza ili
kupata fedha.
Mheshimiwa
Spika, kitendo cha waziri wa maliasili na utalii kumwalika nchini
mwandishi aliyesemwa kuwa ametoa taarifa za uongo na kulichafua taifa,
ili ajithibitishie kuwa Tanzania ni safi katika matukio ya ujangili,
Bwana Martin Fletcher, na kumtembeza katika sehemu mbalimbali nchini
ikiwa na nia ya kumfunga mdomo(damage control), haikusaidia bali
ilivumbua uchafu mwingi na huu wote umewekwa wazi katika vyombo vya
habari vya kimataifa na kuendelea kuonesha uozo wa Serikali katika
kushughulikia tatizo la ujangili nchini.
Mheshimiwa
Spika, imeelezwa kuwa Raisi ameshindwa kusimamia suala hili vizuri kwa
kuwa wanaohusika na ujangili ni watu wake wa karibu ama rafiki zake.
Aidha, taarifa hizo zimeendelea kubana kauli za Waziri Nyalandu za kuwa
anawafahamu majangili kwa majina na kuwataka majangili hao kuacha
ujangili ama watawachukulia hatua za kisheria. Maswali yanayoulizwa, je,
ni kwa nini waziri hawataji watu wanahousika na ujangili? Pili,
inakuaje waziri anawajua kwa majina na hata sehemu wanazokaa, lakini
anashindwa kuwachukulia hatua? Inakuaje waziri, awabembeleze watuhumiwa
wakati kuna sheria, kanuni na taratibu za kuwachukulia hatua wahalifu?
Ni nini kipo nyuma ya pazia katika kuwalinda na kuwaficha watuhumiwa wa
ujangili?
3.1 Kukosekana kwa maafisa utalii katika balozi mbalimbali.
Mheshimiwa
Spika, kuna taarifa kuwa katika balozi zetu mbalimbali na muhimu
ulimwenguni kumekuwa hakuna maafisa utalii ambao watakuwa na jukumu la
kuhakikisha kuwa wanaweza kuhakikisha kuwa tunapata watalii wa kutosha
kwa ajili ya kuinua pato la taifa letu.
Mheshimiwa
Spika, katika ubalozi wa Tanzania –Berlin ni kati ya balozi kubwa
ulimwenguni ambao hauna afisa utalii pamoja na ukweli kuwa ubalozi huu
unahudumia nchi nyingine za
Poland,Austria,Hungary,Frankfut,Uswis,Romania,Bulgaria ,Slovakia na
Jamhuri ya Czech , kwa kipindi kirefu sana ubalozi huu umeomba kupatiwa
afisa utalii kutoka wizara ya mambo ya nje lakini mpaka leo hawajaweza
kupelekewa maafisa hao kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya
uchumi ambayo ndio msingi wetu wa diplomasia ya kimataifa .
Kambi
ya Upinzani, inataka kupata majibu ni lini serikali itawapeleka
wataalamu hao katika ubalozi huu kwa ajili ya kuimarisha sekta ya utalii
kwenye nchi zote muhimu ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika sekta ya
utalii katika taifa letu. [1]
4.0 BIASHARA HARAMU YA NYARA ZITOKANAZO NA WANYAMAPORI NA KUKITHIRI KWA TATIZO LA UJANGILI NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kumekuwa
na ongezeko kubwa na watu wanaojishughulisha na uwindaji na biashara ya
nyara za Serikali bila bila kuwa na kibali au leseni toka mamlaka
zilizowekwa kisheria. Kwa mujibu wa sheria ya wanyapori kifungu
cha 80(1) sehemu ya 10 “mtu yeyote haruhusiwi kujihusisha na biashara
ya nyara (trophies) bila kuwa na leseni ya biashara ya nyara (trophy
dealer license). Na kifungu cha 80(2) kinampa Mkurugenzi wa Idara
ya Wanyamapori mamlaka ya kutoa leseni ya biashara ya nyara kwa mtu
yeyote ambaye ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya
kupokea maombi kwenye fomu maalum na kutimiza masharti yaliyowekwa ikiwa
ni pamoja na kulipa ada zilizopangwa.
Mheshimiwa
Spika, leseni ya biashara ya nyara inayotolewa katika Kifungu hiki
haimruhusu mhusika kuwinda, kuua au kupiga picha mnyama yoyote, badala
yake inamruhusu kukamata, kutengeneza bidhaa inayotokana na nyara,
kununua au kuuza nyara – 80(3)”[2].
Mheshimiwa
Spika, licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, bado wanyama wetu wanaendelea
kuuwawa kwa kasi ya ajabu. Aidha, kumekuwepo kwa taarifa zinazoonyesha
kuwepo kwa mtandao mpana wa wahusika wa biashara ya wanyama pori na
bidhaa za wanyamapori kutoka katika nchi kadhaa kama vile, Kenya,
Msumbiji, DRC, Namibia na Afrika ya Kusini.
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Lazaro Nyalandu aliyoyatoa mbele ya Waandishi wa Habari wakati akiwa
Naibu Waziri wa Wizara hii katika Hoteli ya Mount Meru – Arusha mwaka
jana, ni kwamba; kwa kipindi cha miaka mitatu, iliyopita tembo 31348
sawa na asilimia 42 walitoweka katika hifadhi ya Selous na Mikumi na
kwamba kuna mtandao wa kijangili wa kimataifa (Sophisticated
International Syndicate) unaofanya kazi hapa nchini. Aidha alitoa agizo
kwa bodi ya wadhamini ya mamlaka ya hifadhi za taifa (TANAPA) itoe
maelezo ya kina kuhusu kuwepo watumishi wa ndani ya mamlaka ya hifadhi
wanaosadikiwa kushirikiana na majangili hao kuendesha ujangili ambao
unahatarisha hifadhi zetu na sifa ya nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika, Waziri Nyalandu aliirudia kauli hiyo mkoani Iringa, mwezi
Juni, 2013 wakati wa kikao cha siku mbili cha wadau wa ulinzi wa
maliasili juu ya ujangili wa tembo katika mikoa ya Nyanda za juu na
kuahidi kwamba majina ya majangili yakiwemo ya vigogo wanaojihusisha na
ujangili wa tembo yatatangazwa hadharani, lakini mpaka sasa hakuna
majina yoyote yaliyotangazwa hadharani.
Mheshimiwa
Spika, utafiti uliofanywa na Tanzania Wildlife Research
Institute-TAWIRI katika mbuga ya hifadhi ya Selou na Mikumi inaonyesha
kuwa idadi ya Tembo imeshuka kutoka 74,900 mwaka 2006 hadi kufikia
43,552 mwaka 2009. Hii ikiwa na maana kwamba kwa kipindi cha miaka
mitatu takribani asilimia 42 ambayo ni Tembo 31,348 katika hifadhi mbili
tu waliuawa na majangili[3].
Hii ni hatari kubwa sana na kwa kutilia maanani kuwa Tembo mmoja
anapatikana baada ya miaka miwili (yaani Tembo hubeba mimba kwa kipindi
cha miaka miwili ndipo azae)
Mheshimiwa
Spika, biashara haramu ya nyara zitokanzao na wanyamapori hususan tembo
imechangia sana ujangili wa kutisha wa tembo kiasi kwamba idadi ya
tembo imepungua mno kiasi cha kuwafanya tembo wawe miongoni mwa jamii ya
viiumbe waliopo hatarini kutoweka kabisa (endangered species). Nasema
hivi kwa sababu idadi ya tembo kwa uchache, waliokuwepo katika nchi za
Kiafrika kwa miaka ya sabini walikuwa ni takribani milioni moja na
laki mbili (1,200,000) lakini kwa sasa wamebakia wasiozidi laki tano[4]
Mheshimiwa
Spika, hali ya ujangili nchini imefika pabaya na ina kiasharia kibaya
kwa miaka michache ijayo. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010, jumla ya
tembo 10,000 waliuwawa Tanzania, ikiwa ni sawa na wastani wa tembo 27
kwa siku. Mwaka 2012 pekee, tembo takribani 23,000 wameuwawa kwa mwaka
ambayo ni sawa na tembo 63 kwa siku. Hii ni sawa na ongezeko la 57% kwa
kipindi cha miaka 2. Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na tembo kati ya
150,000 na 170,000. Kutokana na takwimu hizi, ikiwa Tembo 63 wanauwawa
kwa siku, ni dhahiri kwamba kwa kipindi cha miaka 7 ijayo Tembo hawa
watakuwa wameuawa wote.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa
la kupamba na madawa ya kulevya na uhalifu (United Nation’s Office on
Drugs and Crime- UNODC-), inaonyesha kuwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa
la Sahara na nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ni wasambazaji wakubwa
wa bidhaa haramu za wanyamapori kwenye soko la China, Marekani na baadhi
ya nchi katika bara la Ulaya. Bidhaa hizo za wanyamapori ni pamoja na
pembe za ndovu, pembe za faru, ngozi za chui na simba na viungo
mbalimbali vya wanyamapori. Kwa mujibu wa utafiti huo ni kwamba mununuzi
hulipa kiasi cha dolla za kimarekani 2,500 kwa kila pembe moja ya faru.
Mheshimiwa
Spika, tatizo la Ujangili limekuwa gumu kumalizwa kabisa kwa kuna
taarifa zinazohusisha askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi
katika matukio ya ujangili na biashara haramu ya nyara na taarifa hizo
zimeripotiwa sana na vyombo vya habari, lakini cha kusikitisha ni kwamba
hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari wa majeshi hayo (yaani
jeshi la polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania). Mpaka sasa Jeshi la
Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania hawajakanusha taarifa hizo jambo
linaloashiria kwamba pengine taarifa hizo ni za kweli.
Mheshimiwa Spika, taarifa za baadhi ya askari walioripotiwa na vyombo vya habari kuhusika na ujangili ni kama ifuatavyo:
- Mnamo Tarehe 7 January 2013, Gazeti la habari leo lilitoa taarifa za askari wawili kujihusisha na biashara ya meno ya tembo na kuhusishwa na mauaji ya faru katika mbuga ya Serengeti na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka Serikalini juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari hao.
- Mnamo Januari 20, 2013 Sajenti wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Azizi Athuman Yusufu alikamatwa mkoani Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu na bunduki aina ya Riffle yenye namba 458 huku akitumia gari ya mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha nchini.
- Tarehe 23 Julai, mwaka 2013, walikamatwa watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majangili , wakiwamo askari watatu wa Magereza Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wakiwa na gari la Magereza aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STK 4394 lililokuwa limepakia nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55. Nyara hizo zilikuwa ni pamoja na Twiga wawili, Pundamilia wawili, Swala, Palapala majike wawili na Mbuni wawili.
Mheshimiwa
Spika, Biashara haramu ya pembe za ndovu imevuka mipaka ya nchi na
imeanza kushamiri katika ukanda wa Afrika ya Mashariki jambo ambalo
linatishia kutoweka kabisa kwa wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha
utalii. Taarifa katika mtandao wa habari wa “Annamiticus” (www.annamiticus.com)
zinasema kwamba mwaka 2012, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania
yalikamatwa huko HongKong yakiwa yamebeba tani 4 (Kilo 4,000) za pembe
za ndovu.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa
limeandikwa “plastic scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya
plastiki lakini baada ya kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe
halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na
nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa. Kontena lililotoka Kenya
lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage aina ya roscoco,
lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za ndovu sawa
na kilogramu 1,884.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo, wingi wa pembe hizi za ndovu
zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo takriban 600 kwa uchache
waliuwawa.
Mheshimiwa
Spika, mwezi Aprili,2013 kontena lingine lilikamatwa likiwa
limesheheni pembe za ndovu 113 huko China zenye thamani ya Dola za
Kimarekani 400,000.Kontena hili liliandikwa kwamba limebeba vipuri
(spareparts) toka Burundi. Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna
uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na
hivyo kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo
waliouwawa Tanzania.
5.0 MAENDELEO YA SEKTA YA WA WANYAMAPORI NCHINI
Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya wanyamapori katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu ni mkubwa sana. Takwimu[5] zinaonyesha
kuwa uwindaji wa kitalii kwa miaka mitatu kati ya 2009 na 2012
uliingiza shilingi bilioni 91. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Maliasili na
Utalii kupitia idara yake ya Wanyamapori inatakiwa kuilinda na
kuiendeleza sekta hii ili iendelee kuchangia zaidi katika uchumi wetu.
Mheshimiwa
Spika, katika muktadha wa kuilinda na kuiendeleza sekta ya wanyamapori,
Bunge lilitunga Sheria ya Uhifadhi ya 2009, ambayo inatumika pamoja
na sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 ili kuratibu na kudhibiti shughuli
za uwindaji wa wanyamapori kwa namna ambayo sekta ya wanyampaori
inakuwa endelevu.
Mheshimiwa
Spika, ulinzi wa Sekta ya wanyamapori ni muhumu kwa kuwa sekta
inachangia ukuaji wa uchumi katika Nyanja mbalimbali. Kwa mfano
wanyamapori ni kivutio kikubwa cha watalii ambao hutoa fedha nyingi za
kigeni wajapo kutalii hapa nchini kwa ajili ya kutazama na kuwapiga
picha wanyama hao. Aidha sekta ya wanyama pori inachangia maendeleo ya
kiuchumi na kijamii kwa kutoa ajira kwa wananchi na pia kukuza soko la
bidhaa za ndani.
Mheshimiwa
Spika, licha ya umuhimu wa sekta hii, Serikali imekuwa haifuatilii
makampuni ya uwindaji yenye leseni kuona kama wanafuata sheria ya
Uhifadhi wa Wanyamapori ya 2009. Matokeo ya udhaifu wa Serikali katika
ufuatiliaji, kumekuwa na uvunjaji mkubwa wa sheria jambo ambalo
limesababisha uwindaji ufanyike kiholela. Kwa mfano, Kampuni ya Uwindaji
ya Green Miles Safaris Limited imekuwa ikiwakimbiza na kuwakamata
watoto wa wanyamapori pindi wanapozaliwa kinyume na kifungu cha 19(1)
cha Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Aidha Sheria hiyo inapendekeza adhabu
ya kifungo cha miaka mitano gerezani na au faini kati ya shilingi
500,000/= hadi shilingi 2,000,000/=
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba Kampuni hii ya Green
Miles Safaris Limited ilishapewa zuio na Mahakama la kufanya uwindaji
kutokana na uwindaji usiozingatia sheria lakini Kampuni hiyo ilipita
mlango wa nyuma na kuomba kilbali cha uwindaji kwa Mkurugenzi wa
Wanyamapori na Mkurugenzi akatoa kibali na hivyo wote wawili wakapuuza
uamuzi wa Mahakama.
Mheshimiwa
Spika, Kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited, pamoja na uhalifu
mwingi inaoufanya katika mbuga zetu wakati wa uwindaji, imekuwa
ikilindwa na Serikali ndio maana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
Upinzani Bungeni inashawishika kuamini kwamba Serikali ndio chimbuko la
tatizo la Ujangili na uwindaji haramu wa wanyamapori hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo mbele ya
bunge hili ni kwa nini haijaichukulia Kampuni ya Uwindaji Green Miles
kwa kufanya uwindaji haramu hapa nchini?
Mheshimiwa
Spika, Tatizo kubwa la Maendeleo ya Sekta ya Wanyapori ni kwamba
Serikali huwa haifuati hata mapendekezo yanayotolewa na Kamati za
zinazoudwa na Serikali yenyewe. Kwa mfano, mwaka 2006, aliyekuwa Waziri
wa Maliasili na Utalii kwa wakati huo Mheshimiwa Anthony Mwandu Diallo
(Mb), aliunda Kamati ya Wataalam ambayo aliitaka ifanye uchambuzi wa
kina wa shughuli za uwindaji wa kitalii nchini. Uchambuzi huo ulitakiwa
uzingatie utendaji kazi katika shughuli za uwindaji wa kitalii,
mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa na matatizo yanayoikabili tasnia hiyo.
Hatimaye, Kamati ilitakiwa kumshauri Mheshimiwa Waziri namna ya kuleta
mabadiliko ndani ya sekta hiyo kwa minajili ya kulinda uhifadhi,
kuwawezesha wananchi kushiriki katika uwindaji wa kitalii kwa lengo la
kuongeza ufanisi na tija ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika
kuondoa umaskini na kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Hadidu za rejea kamati hiyo ilizopewa ziliitaka Kamati:[6]
(i)
Ipitie utaratibu wa sasa wa uombaji na ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji
wa Kitalii pamoja na chombo chake cha ugawaji kuona kama havibagui wala
havisababishi malalamiko kwa wadau mbalimbali;
(ii)
Ichambue kwa makini vigezo na masharti yaliyopo yanayohusu ukaguzi wa
uwezo wa Kampuni za Uwindaji zinazowasilisha maombi kwa ajili ya
Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama yanafaa kwa mazingira ya sasa;
(iii)
Ichambue Mikataba mbalimbali ya kampuni za uwindaji; ya zamani na
inayoendelea kwa lengo la kujiridhisha kama inafaa au ina upungufu
unaohitaji marekebisho ili kulinda uhifadhi na maslahi ya umma.
(iv)
Iangalie Kanuni za Uwindaji wa Kitalii na zile za Utalii wa picha
pamoja na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 na kushauri namna ya
kuondoa migongano ambayo imejitokeza baada ya kuruhusu utalii wa picha
kwenye maeneo ya uwindaji wa kitalii.
(v)
Ichambue Sera na Sheria zinazohusiana na Wanyamapori na Utalii, na
Kanuni za Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama Wananchi wanafaidika na
uwindaji huo wa kitalii.
(vi)
Ichambue utaratibu wa ukusanyaji mapato, kubaini njia ambazo zitaongeza
maduhuli ya Serikali, na kutathmini utaratibu wa ugawaji vitalu kwa
njia ya zabuni.
(vii)
Mwisho, Kamati iangalie uwezekano wa Serikali kuwawezesha Wananchi
kushiriki kikamilifu katika tasnia hii ya uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Kamati hiyo yalikuwa ni kama ifuatavyo:
- Kuboresha utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa kuipa Kamati ya Ugawaji Vitalu nguvu za kisheria na kwa kupanua uwakilishi wake.
- Kuunda Wakala wa Serikali wa kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii badala ya Idara ya Wanyamapori.
- Kuangalia upya umiliki wa vitalu ili kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika uwindaji wa kitalii kwa njia ya ubia na baadaye kumilikishwa vitalu wakati wageni na wananchi watafanya kazi ya kuwindisha.
- Serikali iwawezeshe Wawindaji Bingwa wa Kitanzania ili waweze kumiliki vitalu na kutumia ujuzi na uzoefu walionao. Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kwa kuzungumza na mabenki ili wapunguze riba ya kukopa fedha benki na kuruhusu matumizi ya vitalu kama dhamana. Pia wawindaji bingwa waanzishe bodi yao ya kitaalam.
- Kuthamini vitalu vya uwindaji wa kitalii na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya Serikali.
- Kuweka ukomo wa umiliki wa kitalu wa vipindi viwili vya miaka mitano ili ili kuruhusu waombaji wapya.
- Kuboresha taarifa za sekta ya Wanyamapori kwa kuweka taarifa zote muhimu zinazohusu shughuli za uwindaji wa kitalii kwenye Tovuti ya Idara.
- Idara iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya vitalu kwa kuanzisha chombo huru cha kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza
Bunge hili ni kwa kiwango gani mapendekezo ya Kamati hiyo
yametekelezwa na ni mangapi ambayo bado kutekelezwa na ni kwanini?
6.0 UTALII NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA
Mheshimiwa Spika,
Kwa
eneo kubwa la ardhi lililofunikwa na wingi wa misitu pamoja na aina
mbalimbali za maua na viumbe, Tanzania ni mojawapo ya vivutio vikubwa
vya utalii barani Afrika. Nchi yetu ina raslimali nyingi asilia ikiwemo
pamoja na maeneo mengi ya nyika za mapori yenye aina nyingi za banoai.
Mheshimiwa
Spika, Miongoni mwa vivutio vya utalii ni pamoja na Mbuga za wanyama ,
hifadhi za taifa, hifadhi zilizozuiliwa na maeneo ya kihistoria. Hata
hivyo kwa sababu ya ongezeko la joto, baadhi ya hivi vivutio ikiwemo
theluji katika kilele cha mlima Kilimanjaro iko katika hatari ya
kupotea. Na baadhi ya wanyama katika mbunga zenye ukame mkubwa wameanza
kupungua na kuathirika.
Mheshimiwa
Spika, Licha ya kuwa na neema ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, bado
sekta ya utalii inakabiliwa na chamgamoto kadhaa, zikiwa ni;
(i)
Uendelezaji wa kazi zitakazohakikisha kuendelea kuwepo kwa vivutio
mbalimbali vya utalii kwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi;
(ii)
Ukarabati wa miundombinu kama vile barabara, madaraja, kambi za watalii
na upatikanaji wa umeme kwa ajili ya watalii wa mbugani;
(iii)
Uwezo mdogo wa idara zinazohusika kusimamia, kulinda vivutio vya
utalii, kama vile kuendesha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, inaamini kabisa tatizo la umeme katika
vivutio vya utalii vilivyopo mbugani, suluhisho ni kutumia umeme wa jua
(solar energy), hili ni rahisi katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa
Spika, kama ambavyo nitaonyesha hapo baadae makusanyo yanayopatikana
kutoka sekta ya utalii hayana uwiano wa moja kwa moja na uwekezaji
katika sekta hiii. Ndiyo sababu kubwa ya mapato ya sekta kutokuakisi
vivutio tulivyonavyo hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, uwekezaji katika Sekta ya Utalii ni suala lenye tija kubwa
katika uchumi wetu kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi
wa Taifa licha ya uwekezaji mdogo uliofanyika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa
Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika maeneo yote ya
hifadhi zetu kwa sasa kuna kuna hoteli zenye uwezo wa kutoa huduma za
malazi (carrying capacity) kwa watu 6,681 ambapo kwa miaka mitano ijayo
idadi hii itafikia uwezo wa kulaza watu 8,421. Hiki ni kwango kidogo
sana cha huduma za malazi kiasi kwamba tunapoteza fursa ya kunufaika
katika sekta ya utalii.
Mheshimiwa
Spika, japokuwa uwekezaji katika sekta ya utalii ni mdogo lakini sekta
imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wetu. Kwa mwaka 2011 utalii
na usafiri wa kitalii ulichangia asilimia 13 kwenye pato la taifa na
kuchangia takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha, Mpango
unaeleza kuwa lengo ni kuongeza wageni kwa asilimia 40 kutoka wageni
671,886 kwa sasa hadi 940,640 ifikap June 2016. Aidha Mpango unalenga
pia kuzidisha siku za mtalii kutembelea maeneo yenye vivutio vya kitalii
nchini kutoka siku wastani wa siku 11 za sasa hadi wastani wa siku 18[7].
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa tathmini ya
mpango huo ili wananchi wajue tumefanikiwa kwa kiwango gani katiaka
kuboresha sekta ya wanyamapori.
Mheshimiwa
Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ya ndani ya nchi,
uwekezaji katika ujenzi wa hotel kwenye maeneo muhimu ya utalii kama
vile kwenye hifadhi, mikoa inayozunguka mlima Kilimanjaro kutasaidia
sana kuvutia watalii. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuboresha miundo mbinu ya usafiri hasa wa anga ili na kujenga hoteli za
viwango vya Kimataifa katika maeneo yenye vivutio vya watalii ili
kuvutia mashirika ya mengi ya ndege toka nje kuja hapa.
Ni
rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Serikali kwamba ifufue shirika letu
la Ndege la Taifa ili tuweze kumudu ushindani katika usafiri wa anga na
hapohapo kuongeza idadi ya watalii katika nchi yetu. Uwanja wa Ndege wa
Kilimanjaro na ule wa Julius Nyerere Dar es Salaam vikiboreshwa vinaweza
kuwa ni kitovu cha mashirika mengi ya kimataifa kubadilishia wasafiri
kama kuna mkakati makini.
Mheshimiwa
Spika, watalii toka nje wanapenda sana kupanda ndege za nchi
wanazotembelea zaidi kuliko kupanda ndege za kuunganisha. Kwa njia moja
au nyingine usafiri huo unawapunguzia gharama. Mfano mzuri ni miaka ya
themanini wakati Air-Tanzania ilipokuwa inafanya safari zake nchi za
Ulaya, watalii wengi walikuwa wanakuja kwa ndege zetu. Hoja ni kwamba
Serikali ina mkakati gani wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATC)
Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Serikali kuingia ubia na makampuni
binafsi kupitia mpango wa Private Public Pertnership – ( PPP) ili
kuboresha huduma za usafiri wa anga hapa nchini ambao unachoche watalii
wengi kuja kwa kuwa kuna usafiri wa moja kwa moja.
7.0 SEKTA YA MISITU
Mheshimiwa
Spika, misitu ina nafasi muhimu ya kumeza hewa ukaa duniani wakati
ikizuia uharibifu wa udongo/ardhi. Ukataji miti na uondoaji misitu
uliokithiri unachangia katika ongezeko la uzalishaji wa hewa ukaa
Tanzania. Kupitia misitu mingi tuliyonayo Tanzania imeendelea kutoa
huduma ya kumeza hewa ukaa duniani, bila ya kuwepo utaratibu wowote wa
kimataifa kutoa fidia yoyote.
Mheshimiwa Spika, mbali ya kuwa na misitu mingi, kumekuwepo na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya misitu, nazo ni:
a) Kufanya uendelezaji wa misitu kama raslimali ya kumeza hewa ukaa na kuinufaisha jamii inayoizunguka;
b) Kuthibiti ubora na uendelevu wa misitu
c) Jamii inayoizunguka misitu kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani;
d) Ujenzi wa uwezo wa kufanya tafiti za uendelezaji misitu nchini;
e) Uendelezaji wa njia bora zinazowezesha jamii inayozunguka misitu kunufaika na raslimali hiyo.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na changamoto hizo, zinazoikabili sekta hii ya misitu,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka kuhakikisha kwa kadri misitu ya
Tanzania inavyoendelea kutoa huduma ya kimataifa ya kumeza hewa ukaa
duniani, hivyo ni lazima nchi na wananchi wetu tunufaike kwa kupata kazi
na teknolojia zinazochangia maendeleo endelevu.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na hilo ni kwamba, ni muhimu Serikali kuhakikisha
unajengwa uelewa kwa jamii na wadau wa misitu juu ya uwepo wa fursa za
kutumia uwezo wa misitu kumeza kumeza hewa ukaa kama chanzo cha
kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani. Kuhamasisha ongezeko la
matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati ya kupikia na kuchemshia na
kupunguza msongo kwenye misitu yetu kwa hitaji hilo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa katika kuhamasisha hilo, ni
muhimu kuwepo kwa misitu mfano na miradi mfano katika ngazi za wilaya
na vijiji ili wananchi waone jinsi misitu inavyoweza kuwanufaisha
wananchi wanaozunguka misitu mfano hiyo. Hili linawezekana kama mipango
na umakini katika utekelezaji wake utakuwepo.
Mheshimiwa
Spika, uwekezaji katika kilimo cha miti ni mojawapo ya kilimo ambacho
kwa muda mrefu kinaweza kuleta tija kubwa kwa wananchi hasa hapa nchini,
uwekezaji huu unakabiliwa na chamgamoto kubwa ya kukosekana kwa mikopo
ya muda mrefu na ambayo inaweza kuwa-accommodate wakulima ambao hawana
dhamana ya kuweka zaidi ya umiliki wa kimira wa ardhi husika, jjambo
ambalo halikubaliwi na taasisi za fedha.
Mheshimiwa
Spika, utaratibu huu wa kilimo cha miti ni maarufu sana katika mikoa ya
Iringa na Njombe, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza
Bunge ni utaratibu gani hadi sasa ambao wakulima wadogo hasa wa miti
wanasaidiwa kupata mikopo ya muda mrefu katika kukabiliana na tatizo
hili la uwepo wa hewa ukaa na kuongeza kipato.
8.0 MAPITIO YA BAJETI KWA IDARA NA VITENGO VYA WIZARA
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 wizara ilitarajia kukusanya maduhuli
ya jumla ya shilingi bilioni 148.97 kutoka katika Idara na taasisi
zilizo chini yake. Mwaka huu wa fedha wizara inatarajia kukusanya jumla
ya shilingi bilioni 144.6, ambayo ni pungufu ya shilingi bilioni 4.37
kwa kulinganisha na makadirio ya mwaka 2013/14.
Mheshimiwa
Spika, randama inaonyesha kuwa Idara ya wanyamapori kwa kipindi cha
mwaka 2013/14 ili kadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.65,
Lakini hadi mwezi Machi, 2014 ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi
bilioni 8.92 ambayo ni sawa na asilimia 31.13 ya malengo. Aidha, kwa
mwaka wa fedha 2014/15 Idara ya Wanyamapori imepanga kukusanya jumla ya
shilingi bilioni 15.55 kutoka kwenye vyanzo vyake vilivyo chini ya
idara. Makadirio haya ni pungufu ya shilingi bilioni 13.1 kwa
kulinganisha na mwaka 2013/14.
Mheshimiwa
Spika, kwa takwimu hizo ni kwamba Sekta ya Maliasili na Utalii
inashuka kimapato. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza
sababu zilizofanya mapato yatokanayo na makusanya ya maduhuli kwa shuka
kwa kiasi kikubwa namna hiyo. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Takwimu
zilizotolewa na taarifa ya uchunguzi maalum ni kwamba kwa kipindi cha
kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 Idara ilikusanya shilingi bilioni 91 na
hali halisi ni kwamba uwezekano kukusanya zaidi ni mkubwa zaidi.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu matumizi ya kawaida, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi
bilioni 19.163 kwa ajili ya matumizi ya Idara hiyo, ambayo ni sawa na
asilimia 22.7 ya makusanyo yake. Lakini hadi mwezi machi 2014, Serikali
imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.161 tu. Swali hapa ni kwamba idara
itawezaje kujiendesha ikiwa fedha iliyotolewa ni kidogo namna hiyo?
Ikumbukwe kwamba Idara hii inasimamia taasisi/vyuo na wakala zipatazo
sita ambazo ni TANAPA, NCAA, TAWIRI,CAWM-Mweka, PWTI na CBCTC ambazo
zinahitaji fedha za kutosha kuziendesha.
Mheshimiwa
Spika, fedha za maendeleo zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye
sekta ya wanyamapori, ni kwa miradi miwili tu ambayo ni mradi wa
KILORWEMP unaotekelezwa kwa ushirika kati ya Tanzania na Serikali ya
Ubelgiji. Mwaka 2013/14 zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 1.82,
lakini hadi Machi 2014 shilingi milioni 310 ambazo zilitoka Serikali ya
Ubelgiji.
Mheshimiwa
Spika, mradi wa pili ni ule wa Kulinda ushoroba wa Selous-Niassa, ambao
unatekelezwa kwenye wilaya za Namtumbo na Tunduru kwa kushirikiana na
Serikali ya Ujerumani. Kwa mwaka jana hakuna fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14 Idara ya Utalii ilikadiriwa kukusanya
jumla ya shilingi bilioni 16.896 lakini hadi mwezi mach, 2014 ilikuwa
imekusanya shilingi bilioni 3.25 ambayo ni sawa na asilimia 19 tu ya
matarajio kwa mwaka. Aidha, fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya Matumizi
ya kawaida kwa idara na Taasisi zilizo chini yake ni shilingi bilioni
12.1, lakini hadi Machi, zilikuwa zimetolewa shilingi bilioni 3.36.
Mheshimiwa
Spika, mwaka wa fedha 2014/15 idara hii ya Utalii inatarajia kukusanya
jumla ya shilingi bilioni 16.91. Aidha, kwa maendeleo Iadara hii
imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.2. Kambi Rasmi ya Upinzani
inauliza inakuwaje Idara inakusanya shilingi bilioni 16.91 lakini
uwekezaji unakuwa wa shilingi bilioni 1.2, aidha uwekezaji huo hauna
matokeo ya moja kwa moja na ukuaji wa utalii. Je ni kwa vipi katika
Dunia hii ya ushindani katika sekta ya utalii inaweza kuleta tija na
kuinua uchumi?
9.0 HITIMISHO
Kambi
Rasmi ya Upinzani, haitochoka kuikosoa Serikali kwa kuwa, kwa muda
mrefu sasa katika Wizara hii tumekua tunatoa mapendekezo ambayo
yanabezwa. Na kwa kuwa ni wajibu wetu kuisimamia ipasavyo Serikali ya
CCM, tunazidi kusisitiza kuwa ili sekta ya maliasili na utalii iendelee
kuna haja nzima ya kubadilisha mfumo wa usimamizi, uendeshaji na
utekelezaji wa Wizara, ambao utatoa fursa kwa viongozi waandamizi wa
Wizara pamoja na watumishi kutimiza na kutekeleza majukumu yake bila
mashinikizo ya kisiasa.
Ni
rai yetu kuwa, Serikali itayafanyia kazi mapungufu yote ambayo tumekua
tukiyasema kwa muda mrefu sasa na kuisimamia ipasavyo sekta hii hili iwe
mhimili wa uchumi kwa taifa kwa kuongeza mapato pamoja na kutoa nafasi
za ajira kwa wananchi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Mch. Peter S. Msigwa (MB)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Maliasili na Utalii.
13.05.2014
[1] ripoti ya CAG 2012/2013 pg 148.
[2] Sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009
[3] www.reuters.com/video/feuters-tv
[4] Haken, J. (2011), “Transnational Crime in the Developing World” in the Global Financial Integrity Journal of February, 2011.
[5] Ripoti ya CAG-ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi maalum kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Machi, 2014
[6] Wizara
ya maliasili na utalii- Taarifa ya kamati kuhusu uboreshaji wa
tasnia ya uwindaji wa kitalii Tanzania, JUNI, 2006
[7] Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011 – 2016