Flatnews

Gharama za maisha zapaa Samunge



Maelfu ya vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wapo Samunge kuchimba dhahabu katika Mto uliokauka wa Karabaline huku wakisema wanapata dhahabu yenye ubora wa juu kuliko ya mahali pengine.
Gharama za maisha katika Kijiji cha Samunge wilayani Loliondo ambako maelfu ya watu wamekimbilia kuchimba dhahabu ambayo imegundulika, zimepanda kiwango cha kutisha hasa chakula na maji.
Katika machimbo hayo mapya maji yanapatikana mbali na eneo hilo, hivyo kufanya ndoo moja ya maji kuuzwa kati ya Sh500 na Sh2,000.
Maji katika eneo hilo lililotapakaa machimbo madogo yasiyo rasmi, yanasambazwa kwa kutumia punda ambao husafiri umbali mrefu na maji hayo pia hutumika kusafishia dhahabu kwa kuwa mto ambao madini hayo yanapatikana umeshakauka.
Kwa upande wa chakula, sahani ya wali inauzwa kati ya Sh3,000 na Sh6,000 huku mguu wa mbuzi ambao wanachinjwa hapo kwa wingi ni Sh8,000.
Mchungaji Mwasapila anena
Akizungumzia hali hiyo jana, Mchungaji Ambilikile Mwasapila aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa wachimbaji hao kupata maji ili kazi yao isisimame.
Mwasapila aliyewahi kukaririwa akisema watu watajaa tena Samunge kuliko wale waliokwenda kwake kunywa kikombe cha dawa ya kutibu magonjwa sugu, alisema kupatikana kwa dhahabu katika eneo hilo ni sehemu tu ya ndoto yake.
Alisema mbali na dhahabu hiyo ya Samunge inayoanza kukusanya watu, bado kuna mambo makubwa yatakayotokea na maelfu ya watu kujaa zaidi.
"Hili la dhahabu sijawahi kulisema lakini kuna mengi yatatokea katika eneo hili la Samunge," alisema.
Kama ilivyokuwa wakati wa tiba hiyo, katika machimbo haya bado hakuna mahala pa kulala, wachimbaji na watoa huduma katika eneo hilo wanalala kwenye mahema na kijijini Samunge.
Huduma za afya zinapatikana jirani na eneo la machimbo ambako safari hii kuna zahanati.

Post a Comment

emo-but-icon

item