ADEN RAGE HAKUWA NA THAMANI YA UONGOZI WA SOKA?
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/aden-rage-hakuwa-na-thamani-ya-uongozi.html
Kumalizika kwa kipindi cha uongozi, kwa mwenyekiti
wa mwisho wa klabu ya soka ya Simba SC, Mh. Ismail Aden Rage, kumezua mgawanyiko
wa maoni juu ya utawala wa miaka minne ya uongozi kama alifanya vizuri, au
alianguka.
Jambo la
muhimu kwa sasa ni wanachama wa klabu hiyo ni kutafakari, kabla ya kufanya machaguo
mapya ya utawala wa miaka minne, ijayo.
Simbaya 2014-2018,inahitaji nini? Jibu lake
lapaswa kuendana na swali, Je, ni kina nani hasa wanaweza kuwa dira ya matarajio
yanayokusudiwa?.Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatilia kuhusu utawala wa miaka minne
ya Rage, na kujiaminisha kuhusu uwezo wake. Alishindwa kuwa mkweli katika mambo
yake mengi aliyokuwa akiwaahidi wanachama wa klabu yake, kama mwenyekiti alishindwa
kukabiliana na changamoto nyingi za ahadi zake hewa, ambazo ziligeuka na kuwa '
dhoruba ' zilichangia wengi kukosa imani naye.
Klabu ya soka ya Simba SC, inataraji kufanya uchaguzi
wake mkuu, ambao utawaingiza madaraki, rais wa kwanza wa klabu hiyo, makamu
wake, na wajumbe wa kamati ya utendaji ambao watakuwa na jukumu la kuiongoza timu
hiyo katika kipindi cha miaka minne ijayo. Je, Simba ya kuanzia, mwezi Juni,
mwaka huu hadi, Juni, 2018, inahitaji watu wenye sifa gani?
Wakati, Rage alikuwa na hofu ya kupinduliwa zaidi ya
mara mbili, japo alijionesha mwenye hali ya kujiamini wakati akiitumia katiba ya
klabu hiyo kujinga kama ngao ya kumlinda, bado uwepo wake katika klabu hiyo ulikuwa
na sababu nyingi za kupingwa. Mimi ni mtu, ambaye sikupendezwa na namna mwenyekiti
huyo alivyokuwa akitoa ufafanuzi wa mambo muhimu kuhusu katiba ya klabu, badala
ya kuwaelimisha wanachama wake akaishia kuwatukana kwa kuwaita‘ mbumbummbu’.
Simba, ijayo katika mfumo mpya wa kiutawala haitakiwi kuongozwa na kiongozi mwenye
matusi, ambaye anatumia maarifa yake kujikweza.
Kitu pekee alichofanikiwa katika uongozi wake ni kurudisha
umeme katika jengo la makao makuu ya timu hiyo. Rage, aliendeleza migogoro aliyorithi
kutoka katika uongozi wa Hassan Dalali, na Mwina Kaduguda. Inawezekana aliangushwa
na watendaji wake wa chini, lakini kama Mwenyekiti wa klabu anapaswa kubebeshwa
lawama kuhusu upotevu wa pesa nyingi za klabu ambazo ingeweza kuzipata kutokana
na mauzo ya wachezaji waliouzwa ng’ambo katika miaka minne ya utawala wake.
Kama, kiongozi makini, malipo ya Mbwana Samatta na Patrick Ochan, yangeweza kuifanya
timu hiyo kuwa na uwanja wake walau wakufanyia mazoezi.
Wachezaji hao wawili waliingiza zaidi ya million
300, lakini mapema mwezi uliopita walikuwa wakichangishana walau million 75 ili
kutengeneza uwanja wa kisasa wa kufanyia mazoezi. Rage, aliingia madarakani huku
akijinadi kuwa atasaidia timu hiyo kuwa na uwanja wake, lakini alikiri wazi miaka
miwili iliyopita mbele ya wanachama wa klabu hiyo kuwa kila kitu kinashindwa kufanyika
kutokana na kukosekana kwa million 30 ili kupata hati ya kiwanja chao ambayo gharama
yake ilifikia hadi million 80. Jiulize, pesa za Samatta na Ochan zilifanya kazi
gani, utaambiwa zilitumika kwa mambo mengine.
Wanachama wa Simba hawapaswi kufanya kosa tena kwa
kuchagua watu wasio wakweli, halafu na wenye mipango isiyotekelezeka. Rage
hakuwa na thamani ya uongozi wa soka.
Simba wameshindwa kupata viongozi wenye sifa za kuongoza
klabu yao? Katika kipindi cha miaka 14 sasa, timu hiyo bado inaendeshwa na kikundi
cha watu. Wakati fulani, alikuwepo Kassim Dewji ambaye chini yake, Simba ilikuwa
kali ndani ya uwanja, lakini kama kiongozi wa juu wa klabu aliiacha akaunti ya timu
hiyo ikiwa haina chochote. Katika jitihada za kumpata kiongozi makini walimjaribu,
Michael Wambura, japo alionekana ni kiongozi hodari alikuwa hajachaguliwa na wanachama.
Kwa kujaribu tena, wakaingia, Mzee Dalali, na Kaduguda
ambao chini yao, Simba ilikuwa na ukata, vurugu za mara kwa mara, huku wakitumia
vyombo vya habari kurushiana makombora. Baada ya wote hao kuonekana hawana jipya,
wanachama wa Simba wakaangukia kwa Rage, mwaka 2010, mwanasoka wa zamani wa timu
hiyo. Rage aliingia kwa ' mbwembwe' huku wengi wakiamini kuwa ataipaisha timu hiyo,
lakini ameishia kuwa 'mwanasiasa' ambaye aliingia Simba kwa nia ya kujikuza na kujitangaza
kisiasa.
Rage ameona dalili za kupoteza nguvu na ushawishi kutoka
kwa wanachama ndiyo maana akatangaza mapema kutogombea nafasi hiyo kwa muhula wa
pili. Mwenye pesa siku zote humtafuna asiyekuwa nazo, uongozi uliopita uliitafuna
klabu iliyochoka kiuchumi na kuiacha katika nafasi mbaya ndani ya soka la
Tanzania.Kipindi cha miaka minne ya utawala wa mwenyekiti anayemaliza muda
wake, Rage kimekuwa chenye wakati mgumu ndani
ya uwanja hadi katika nafasi za utalawa. Ndani ya uwanja timu imefanikiwa kushinda
mara moja tu ubingwa wa ligi kuu, 2011/12, mara moja kumaliza katika nafasi yapili,
2010/11, mara moja kumaliza katika nafasi ya tatu, 2012/13, na safari hii wakimaliza
katika nafasi ya nne.
Mei, 29 iwe siku ambayo kila mwanachama atakuwa amejua
ni nani hasa ambaye anaweza kuondoa matokeo mabaya ya timu ndani ya uwanja na kuongoza
safu ya uongozi kuifanya klabu kujitegemea kiuchumi. Simba inahitaji mtu,
ngangari ambaye atatumia jina la timu hiyo kuifanya kuwa taasisi yenye uwezo wa
kusimama yenye na kujithamini katika mikopo mikubwa. Mambo hayo hayawezi kuwepo
kwa mtu alafi, mwenye majivuno na mbishi katika kusikiliza ushauri wa watu wengine.
Simba inaweza kunufaika na logo yake kama watadhibiti bidhaa zote zenye nembo yao
katika masoko ya Tanzania. Inahitaji mtu, jasiri ambaye si tu atakuwa na utajiri
mkubwa, marafiki wenye pesa, mchezaji wa zamani, au mfanyabiashara, Simba inahitaji
mtu mwenye thamani hasa ya uongozi. Muadilifu, msikivu, mwenye busara na uwezo wa
kujiongoza yenyewe, tuachane na mambo ya kina Aden Rage na Mzee Dalali, ni wakati
wa kusimamia matarajio mapya ya siku za mbele.
0714 08 43 08