Palestina yataka muda maalum Israel kuondoka katika ardhi yake
Hakuna sababu ya kuwa na mazungumzo ya amani na Israel hadi pale lengo litakapokuwa kufikisha mwisho miaka 47 ya Israel kulikalia eneo l...
http://samchardtz.blogspot.com/2014/09/palestina-yataka-muda-maalum-israel_27.html
Hakuna sababu ya kuwa na mazungumzo ya amani na Israel hadi pale lengo
litakapokuwa kufikisha mwisho miaka 47 ya Israel kulikalia eneo la
Wapalestina kwa kupanga muda maalum.
Wapalestina wanataka kuwe na muda maalum ambapo Israel itaondoka katika
ardhi ya Wapalestina , amesema rais wa Palestina Mahmoud Abbas
alipolihutubia baraza kuu la Umoja wa mataifa jana Ijumaa (26.09.2014).Wapalestina wanataka kurejea katika majadiliano ya amani na Israel lakini ni pale tu lengo litakapokuwa kufikisha mwisho Israel kulikalia eneo la Palestina na kuhusisha muda maalum wa kufanya hivyo.
"Hakuna uaminifu ama nia thabiti katika majadiliano ambamo Israel inapanga matokeo kupitia shughuli zake za kujenga makaazi ya Walowezi," Abbas amesema, " Muda sasa umefika kwa kumalizwa uvamizi huu wa makaazi. "
Masuala ya msingi hayajaangaliwa
Abbas amesema "duru ya mzunguko wa majadiliano" umeshindwa kuangalia masuala ya msingi.
"Wazo kwamba inawezekana kirahisi tu kurejea katika mfumo wa zamani wa kufanyakazi, ambao umeshindwa mara kadhaa, ni suala lisiloeleweka katika kila hali, ni kosa," Abbas amesema.
Abbas amesema Wapalestina na kundi la mataifa ya Kiarabu limekuwa likifanyakazi kutayarisha mswada katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa "kusukuma mbele juhudi za kupatikana kwa amani." Abu Rdainah , msemaji wa Abbas, amesema Ramallah inataka baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kumalizika kwa ukaliaji wa ardhi ya Wapalestina katika muda wa "miaka miwili ama mitatu."
Wanadiplomasia wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa (26.09.2014)wamesema kuwa Jordan , moja kati ya nchi 15 wanachama wa baraza hilo, bado haijasambaza mswada huo wa azimio kwa niaba ya Wapalestina na kundi la mataifa ya Kiarabu.
Mswada wa azimio la kufikisha mwisho ukaliaji wa eneo la Palestina
Baraza hilo tayari limekuwa likijadili kwa wiki kadhaa mswada mwingine uliotayarishwa na Jordan kuhusu makubaliano yaliyosimamiwa na Misri ya kusitisha mapigano mwishoni mwa mwezi wa Agosti ambayo yamemaliza mapigano yaliyodumu siku 50 katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na Palestina.
Uingereza , Ufaransa na Ujerumani zimependekeza pamoja katika mswada huo kuundwa kwa utaratibu wa kimataifa wa kuangalia usitishaji mapigano pamoja na uchunguzi. Wanadiplomasia wanasema ujumbe kama huo unaweza kutayarishwa na Umoja wa Mataifa ama Umoja wa Ulaya.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Isreal Avigdor Lieberman amesema katika taarifa kuwa hotuba ya Abbas imeweka wazi kwamba rais wa Palestina " hataki na hawezi kuwa mshirika katika suluhisho lolote la maana la kidiplomasia."
"Si bure kwamba Abu Mazen amejiunga na serikali ya pamoja na kundi la Hamas , Abu Mazen anaiunga mkono Hamas na siasa zake za kigaidi na kutoa hadithi juu ya Israel," amesema Lieberman, akimaanisha Abbas na jina lake la utani.
Kabla ya hotuba yake jana Ijumaa , wasaidizi wake walisema atazindua juhudi mpya kwa baraza la Usalama kuweka muda wa miaka mitatu kwa Israel kuondoka katika ardhi ya Palestina iliyokamatwa katika vita vya mwaka 1967. Wameongeza kuwa kukataliwa kwa ombi la Palestina na Umoja wa Mataifa kutasababisha Abbas kuomba uanachama katika mashirika ya kimataifa , ikiwa ni pamoja na mahakama kuu ya kimataifa ya uhalifu.
Hatua hiyo itafungua mlango kwa madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya Israel kutokana na mashambulio yake ya kijeshi katika ukanda wa Gaza na ujenzi wa makaazi ya wayahudi katika ardhi ya eneo la Ukingo wa magharibi ambalo Wapalestina wanataka kwa ajili ya taifa lao.
Hata hivyo hotuba ya Abbas haikugusia juhudi za kujiunga na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ama muda maalum wa kumalizika kwa ukaliaji ardhi ya Wapalestina kunakofanywa na Israel , na kutaja tu "haja ya , kuwa na muda maalum wa utekelezaji wa malengo hayo."
Kujiunga na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kutakuwa ni hatua kubwa ya sera kwa Abbas. Itabadilisha uhusiano wake na Israel kutoka hali mbaya na kuwa uhasama wa wazi, na kuathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na Marekani.
Kiongozi wa Palestina ametishiwa iwapo atajiunga na ICC tangu mwaka 2012, wakati Palestina ilipopata kupanda hadhi na kuwa mtazamaji ambaye si mwanachama katika Umoja wa Mataifa, hadhi inayoruhusu kuwa mwanachama katika vyombo mbali mbali vya kimataifa.
Hata hivyo , Abbas alikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry siku ya Jumanne ambapo alimelezea matumaini madogo kwa juhudi zake katika Umoja wa Mataifa na kwamba hazitaweza kufanikiwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Marekani na Israel zashutumu hotuba ya Abbas
Wakati huo huo Marekani imeshutumu hotuba ya Abbas katika hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa. Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imetoa angalizo kali la kidiplomasia kwa hotuba ya rais wa Palestina Mahmoud Abbas katika hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa akiishutumu Israel kwa uhalifu wa kivita katikati ya mwaka huu katika vita vya Gaza.
Msemaji wa wizara hiyo Jen Psaki amesema hotuba ya Abbas imejumuisha mambo kadhaa ya kuchukiza ambayo Marekani inayapinga na kuyataka kama ya uchokozi, yasiyo na manufaa na hayasaidi juhudi za kurejesha uaminifu kati ya Israel na Palestina.