Viongozi wa Ulaya wataka amani itunzwe
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/viongozi-wa-ulaya-wataka-amani-itunzwe.html
Viongozi wa Ulaya wameshinikiza kuchukuliwa hatua zaidi za kuitunza
amani wakati walipokusanyika Ubelgiji kwa kumbukumbu ya miaka 100 ya
kuvamiwa kwa nchi hiyo na Ujerumani mwanzoni mwa Vita Vikuu vya Kwanza
vya Dunia.
Viongozi wa Ulaya na wafalme waliohudhuria kumbukumbu ya miaka 100 ya
Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Liege ,Ubelgiji. (04.08.2014)
Katika kumbukumbu hiyo ya Jumatatu (04.08.2014) Ubelgiji, Ufaransa na
Ujerumani nchi zilizokuwa mahasimu hapo zamani zimesimama bega kwa bega
kwa moyo wa usuluhishi.Uvamizi wa Ujerumani kwa Ubelgiji uliifanya Uingereza nayo itangaze vita dhidi ya Ujerumani. Mzozo huo ambao hatimae ulizihusisha nchi 40 ulimalizika hapo mwaka 1918 baada ya miaka minne na kusababisha vifo vya watu milioni 16.
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani alikuwa miongoni mwa wageni wa heshima katika kumbukumbu hiyo ya leo iliofanyika katika mji wa mashariki nchini Ubelgiji wa Liege. Amesema amani barani Ulaya haiwezi kuchukuliwa kama ni kitu cha sadaka tu, yaani kilichopatikana bila ya jasho:
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani akihutubia katika kumbukumbu ya miaka 100 ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. (04.08.2014)Rais huyo wa Ujerumani pia amewashukuru wananchi wa Ubelgiji ambao baada ya vita viwili,baada ya kuvamiwa mara mbili na vikosi vya Ujerumani, baada ya kutendewa unyama na kuteseka wameinyoshea Ujermani mkono wa usuluhishi muda mfupi baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Ulaya ina wajibu wa kutunza amani
Rais Francois Hollande wa Ufaransa akizungumza wakati wa kumbukumbu hiyo iliohudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 83 duniani ameitaja mizozo ilioko Ukraine,Iraq,Syria na Ukanda wa Gaza na kusema kwamba ni wajibu wa Ulaya kutuma ujumbe wa amani.
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani aliyesimama (kulia) Rais Francois
Hollande wa Ufaransa aliyekaka kitako (pili-kulia) na Mkuu wa jimbo la
Cambridge mjukuu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza na mke wake
Kate.Liege, Ubelgij. (04.08.2014)Waziri Mkuu wa Ubelgiji Elio Di Rupo yeye amesema hakutakiwi kufanya makubwa kuvunjilia mbali mshikamano na kuamsha mvutano mbaya kabisa, akiwa anakusudia mafanikio waliyopata hivi karibuni vyama vya sera kali za mrengo wa kulia barani Ulaya.
Dhima ya Ubelgiji yapongezwa
Waliohudhuria kumbukumbu hiyo pia wamelitumia tukio hilo kuipongeza Ubelgiji kwa dhima yake katika vita vikuu vya kwanza vya dunia. Kusonga mbele kwa vikosi vya Ujerumani nchini humo kulizuiliwa katika konde zilioko karibu na mji wa magharibi wa Ypres ambapo mamia kwa mamia ya wanajeshi wa nchi washirika na wale wa Ujerumani walipoteza maisha yao.
Mtawala wa jimbo la Cambridge mjukuu wa Malkia wa Uingereza William ameiwakilisha Uingereza katika kumbukumbu hiyo akiandamana na mke wake Kate.
William na Rais Gauck wa Ujerumani walikuwa wanatazamiwa pia kushiriki katika kumbukumbu nyengine tafauti katika makaburi ya kijeshi ya mtakatifu Symphonnen katika mji wa kusini wa Mons ambapo wanajeshi wa Jumuiya ya Madola na wa Ujerumani wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia wamezikwa.
Rais wa Ujerumani pia atazuru mji wa Leuven ambao ulikuwa karibu umeangamizwa kabisa na vikosi vya Ujerumani hapo mwaka 1914 vikiwemo vitabu vya aina yake na nyaraka.
Kumbukumbu ya karne moja ya Vita Vikuu vya Kwanza Dunia inafanyika duniani kote.
