Mkutano wa kilele Afrika, Marekani waanza
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/mkutano-wa-kilele-afrika-marekani-waanza.html
Mkutano wa baina ya viongozi wa Marekani na Afrika unafunguliwa leo
mjini Washington, ukihudhuriwa na zaidi ya marais 40 wa Kiafrika ambapo
hapo Jumatano wakati Rais Barack Obama wa Marekani akapoongoza mkutano
huo.
Rais Barack Obama wa Marekani
Tayari viongozi wakuu kadhaa wa Afrika wameshawasili mjini Washington,
akiwemo Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye alikuwa na mazungumzo na
raia wa nchi yake wanaoishi hapa Marekani. Vile vile marais wa nchi
nyingine za Afrika ya Mashariki na Kati tayari wamepiga kambi kwenye
hoteli za Washington, kabla ya mkutano wa kilele unaotarajiwa Jumatano.Wizara ya Nje ya Marekani inasema kwa ujumla ni marais 47 watakaohudhuria mkutano huo, huku Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na mwenziwe Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone wakifuta ziara yao kutokana na ugonjwa wa Ebola katika nchi zao. Wengi miongoni mwa marais hao wamekuja na wake zao.
Ajenda za mkutano
Rais Obama akitembelea maduka ya vyakula mjini Dakar, Senegal, mwaka 2013.Mikutano hiyo kwa pamoja itazungumzia utawala bora barani Afrika. Hata hivyo, mkutano unaosubiriwa kwa hamu sana hii leo ni ule unaohusu mradi wa umeme barani Afrika, "Power Africa", ambao ulianzishwa na Rais Obama mwaka jana.
Jumanne marais wote watakuwa na chakula cha jioni na Rais Obama na mkewe, Michelle, kwenye ikulu ya White House. Kilele cha mkutano huo ni hapo Jumatano (6 Agosti) kwa mkutano baina ya Rais Obama na marais wote wa nchi za kiafrika, ambao utakuwa na vikao vitatu kwa wakati mmoja - kikao cha kwanza kitahusu maswala ya uchumi na uwekezaji barani Afrika, cha pili kitahusu amani na usalama wa nchi za Kiafrika na mwishowe itakuwa ni kikao kitakachojadili maswala ya utawala bora barani Afrika.
Obama kutokukutana na kiongozi mmoja mmoja
Uchumi unaimarika barani Afrika.Lakini maafisa wa serikali ya marekani wamelezea kwamba mkutano huo unalenga siyo kupanga mikakati kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, bali ushirikiano wa dhati baina ya pande hizo mbili kwani Afrika ni bara ambalo uchumi wake unakuwa kwa kasi.
Viongozi wa mashirika ya kiraia wanaitaka Marekani kuwashinikiza viongozi wa Kiafrika kuhusu utawala bora na matumizi ya rasilimali za bara hilo kwa manufaa ya watu wake.
