Flatnews

Magufuli ahimiza Daraja Kigamboni


NAKAGUA: Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli akipata maelekezo kutoka kwa Meneja Mradi wa Daraja la Kigamboni, Mhandisi Karim Mattaka (kushoto) wakati wa ziara ya waziri huyo kukagua ujenzi wa daraja hilo na vivuko jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory 
  • Dk Magufuli amewamwagia sifa wakandarasi wazawa akisema wanaweza kufanya kazi vizuri kuliko wakandarasi wa kigeni wanapoaminiwa na kupewa miradi ili waitekeleze.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli amewataka watendaji na wakandarasi wanaojenga Daraja la Kigamboni, kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kabla ya Juni mwakani.
Pia, Dk Magufuli amewamwagia sifa wakandarasi wazawa akisema wanaweza kufanya kazi vizuri kuliko wakandarasi wa kigeni wanapoaminiwa na kupewa miradi ili waitekeleze.
Magufuli aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua Kivuko cha Msanga Mkuu, mkoani Mtwara kinachojengwa, Kivuko cha Kigamboni kinachofanyiwa ukarabati na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kamandi ya Wanamaji na ukaguzi wa Daraja la Kigamboni.
Daraja hilo linalojengwa na kampuni ya Kichina ujenzi wake unaelezwa kuwa umekamilika kwa asilimia 60, huku  barabara zake zikiwa zimejengwa kwa asilimia 37, ambapo takriban Sh214 bilioni zitatumika kukamilisha ujenzi huo ulioanza mwaka 2012 ukitarajiwa  kukamilika Januari mwakani kwa  fedha za Serikali na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF).
“Ninawaomba watendaji na makandarasi wote na NSSF mfanye kazi usiku na mchana ili kuhakikisha inapofika Juni mwakani na siyo Julai mlivyosema, daraja hili liwe limekamilika na Rais Jakaya Kikwete aje hapa alifungue yeye mwenyewe kwani ndiye aliyelianzisha,” alisema Dk Magufuli
Kuhusu makandarasi wa ndani, Dk Magufuli alisema Kampuni ya Uholanzi ya Schepsbouw Noord, ilipewa kujenga kivuko cha Msanga Mkuu, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu ilishindwa kukikamilisha hivyo alifukuzwa na kazi hiyo kukabidhiwa mkandarasi mzalendo. “Wazalendo wanaweza, hawa Wazungu hawafai kabisa…,” alisikika akisema Dk Magufuli.
Awali Meneja Mradi wa Daraja la Kigamboni, Mhandisi Karim Mattaka alisema mpaka sasa jumla ya Sh117 zimetumika.

Post a Comment

emo-but-icon

item