Flatnews

KOCHA TAIFA STARS ASHAURI KUPUNGUZA IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI LIGI KUU BARA


Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dr. Mshindo Msolla
KOCHA mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Mzalendo, Mshindo Msolla amesema walimu wa kigeni wanaokuja nchini kufundisha klabu kubwa za ligi kuu hawasaidii kuendeleza soka la Tanzania.
Msolla alisema makocha hawa wanapewa mkataba wa mwaka mmoja au miwili, hivyo wanahangaika kusajili wachezaji nyota wa kigeni ili kupata mafanikio na kuondoka, jambo ambalo linawanyima nafasi ya kuwajenga wachezaji wazawa kwa muda mrefu.
“Hawa walimu wa kigeni wanaokuja klabu zetu kubwa,  hawatusaidii kuendeleza mpirawetu. Katika mkataba wake wa miaka miwili anataka afanikiwe aondoke. Kwa mfano yule kocha wa Yanga, Costadin Papic alitaka kila nyota aletwe”
“Labda naona kidogo Maximo anajitahidi. TFF wao ndio wasimamizi wa mpira, wasichanganyikiwe kwa timu ya taifa kutolewa katika mashindano ya kufuzu fainali za Afrika, wakubali kwasababu hatuna mipango endelevu”.
Kocha huyo aliyeifundisha Taifa Stars mara nyingi kwa vipindi tofauti na mara ya mwisho ilikuwa  mwaka 2005 kabla ya kuja kwa Marcio Maximo  2006 aliongeza kuwa idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni (watano) inasababisha kuathiri timu ya taifa kwasababu wanakuja kuwabana wazawa kupata nafasi ya kucheza.
 
“Timu ya taifa ya Tanzania imeathirika kwasababu ya haya, tumeng`ang`ania kuwa na wachezaji wengi wa kigeni, nikiangalia usajili wa mwaka huu ulivyo kwa timu kubwa tatu (Yanga, Simba na Azam fc), inawezekana kwenye safu ya ushambuliaji wa timu hizi, mchezaji mmoja wa Kitanzania akawepo, haitasaidia kuwajenga Watanzania.” Alisema Msolla.
“Kama una timu tatu zinazotoa wachezaji wa timu ya taifa, halafu katika timu hizo ni mchezaji mmoja tu anayeanza, haiwezi kusaidia. Ushauri wangu idadi ya wachezaji wa kigeni isizidi watatu.”
Msolla alitoa ushauri kwa shirikisho la soka Tanzania, TFF, kuwatumia makocha wazawa waliowahi kufundisha timu ya taifa ili wawe wanampa ushauri kwa kwasababu ya uzoefu wao wa soka la Tanzania.
“Pale TFF kuna kamati ya ufundi na mkurugenzi wa ufundi. Mimi nilishauri, nchi hii ina walimu wengi wazawa waliofundisha timu ya taifa , mwalimu wa timu ya taifa hatapoteza chochote kama tutakaa naye kuweka mipango. Yaani sisi tumsaidie  kwasababu tunawajua wachezaji wetu, na hili halina gharama yoyote.” Alisema Msolla.
“Mwalimu sio mungu, hatutamlazimisha amchague nani, lakini tunamshauri tu na hii itasaidia kwasababu sisi tunawajua wachezaji wetu”.

Post a Comment

emo-but-icon

item