JK AWASHAURI DIASPORA KUJENGA HOJA YA URAIA PACHA NA KUWACHANA NA MATUSI MITANDAONI
Kikwete: Jengeni hoja kutetea Uraia pacha badala ya kupiga kelele mitandaoni tu! TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Rais wa Jamhur...
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/jk-awashauri-diaspora-kujenga-hoja-ya.html
 |
Kikwete: Jengeni hoja kutetea Uraia pacha badala ya kupiga kelele mitandaoni tu!
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewataka Watanzania waishio nje ya nchi na wanaotaka kuona Tanzania
inakubali kuanzisha mfumo wa uraia pacha kutumia muda wao kujenga hoja
za jambo hilo badala ya kupoteza muda kwenye mijadala ya blogu na
kulaumi watu wengine. Rais Kikwete amewataka Watanzania hao kusema
ili wasikike kwa sababu, kimsingi, hoja ya uraia pacha haina nguvu
miongoni mwa Watanzania wanaoishi Tanzania bali hoja hii inatokana zaidi
na msukumo wa Watanzania wanaoishi nje ambao kwa bahati mbaya hawafanyi
jitihada za kutosha kutetea hoja yao. Rais
Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati
alipokutana, akazungumza na kujibu maswali ya Watanzania wanaoishi
Marekani, hasa katika maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya
Virginia, Maryland, New York na hata California katika mkutano
uliofanyika katika Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.
Rais
Kikwete yuko katika ziara ya siku tisa katika Marekani ambako miongoni
mwa mambo mengine atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Marekani na Afrika
ambao shughuli zake zinaanza leo Jumatatu. Mkutano huo, umeitishwa na
Rais Barack Obama wa Marekani na unahudhuriwa na viongozi wa nchi 47
kutoka Afrika.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao kuacha
kupoteza muda kujadili mambo yasiyokuwa na maana na badala yake
kuelekeza nguvu zao katika kujenga hoja yenye nguvu zaidi ya uraia
pacha, jambo ambalo ni moja ya mambo yatakayojadiliwa katika mchakato wa
Katiba mpya.
“Mnashinda kwenye blogu mkijadili mambo ambayo
wenzenu nyumbani wana uwezo mkubwa zaidi kuyajadili kuliko nyie.
Mnajiingiza katika mambo ambayo sisi nyumbani tuna uwezo mkubwa nayo
kuliko nyie. Kwa mambo haya, sisi tunatosha zaidi. Mnaacha kujadili
mambo yanayohusu maisha yenu – kama hili la uraia pacha na mnajiingiza
katika mambo yasiyowahusu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa
sasa upo huu mjadala wa uraia pacha ni hoja yenu. Nyie badala ya
kushiriki katika mjadala huu kwa njia zote, mnashinda kujadili mambo
ambayo hayana maana. Kwanza hoja ya uraia pacha siyo hoja ya watu wengi
nyumbani, siyo jambo linalowahusu. Hata rasimu sina uhakika kama
mmeisoma vizuri na kujua nini kimependekezwa – lakini hata huo muda
hamna. Kazi yenu mnashinda mnajadili mambo yasiyokuwa na maana – nani
kavaa nguo fupi, nani kafanya nini, haya ndiyo mambo yanayochukua muda
wetu.”
Rais Kikwete amesisitiza: “Ushauri wangu ni kwamba
tumieni muda wetu kusaidia kusukuma hoja yenu hii muhimu – ambayo kama
mnavyojua imeingizwa katika rasimu kwa mapendekezo ya CCM kwa sababu
suala hilo halikuwemo katika rasimu ya kwanza.”
Imetolewa na; Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu – Dar es Salaam. 04 Agosti, 2014
|