WATUHUMIWA WAWILI WA UJAMBAZI BENKI YA NMB WAUAWA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/watuhumiwa-wawili-wa-ujambazi-benki-ya.html
Watuhumiwa
wawili wa ujambazi wameuawa jijini Dar es Dalaam na wananchi katika
jaribio la kufanya tukio la uporaji katika eneo la benki ya NMB Wilaya
ya Ilala.Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa
walikuwa wakijaribu kumpora mteja aliyekuwa ndani ya benki hiyo
akichukua fedha kwa kutumia silaha mara baada ya kutoka ndani ya benki
hiyo.Kamishna wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao ambao
idadi yao haijafahamika walifika katika eneo la benki hiyo tawi la
Uwanja wa Ndege wakiwa na pikipiki tayari kufanya tukio hilo.
“Hawa
walikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna watu wenye
pikipiki ambao wanahisi wanataka kufanya uhalifu. Polisi waliweka mtego
nje ya benki lakini waliwashtukia polisi na kuanza kukimbia kila mmoja
kwa njia yake,” alisema.
Alisema
wakati wahalifu hao wakikimbia, mmoja alifyatua risasi kwa lengo la
kupambana na askari, lakini askari hao walifyatua risasi juu kwa lengo
la kumuamuru asimame.
“Walifanikiwa
kumkamata na alipopekuliwa alikutwa na bastola aina ya Browing yenye
namba 230787 iliyotengenezwa nchini Chekoslovakia ikiwa na risasi tatu.
Hata hivyo wananchi waliokuwa wengi waliwazidi nguvu polisi
wakamshambulia.
“Walimshambulia
kwa mawe lakini polisi walifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza hospitali
lakini alifariki akiwa njiani,” alisema Kova.
Alisema
jambazi mwingine ambaye alikimbilia katika eneo la Karakata, wananchi na
askari walimkimbiza, lakini hakusimama hata askari walipopiga risasi
juu kumtaka asimame.
Alisema
baada ya polisi kuona mtuhumiwa huyo anakaidi agizo la kusimama,
walimpiga riasasi miguuni na alianguka na kuishiwa nguvu kabla ya
kufariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Kova
alisema baadaye jioni jana, watuhumiwa wengine watatu walikamatwa.
Aliwataja kuwa ni Salum Seleman (28), Samwel Clips (32) na Said Salehe
ambaye ni mganga wa kienyeji.
Alisema
Seleman na Clips walikamatwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari
baada ya kugundulika kuwa ni watuhumiwa wa ujambazi katika tukio hilo,
ambalo wenzao waliuawa.
“Hawa
walifika kituoni pale wakiwa wamebadili nguo na kujifanya ni wateja wa
kawaida, lakini lengo lao ni kuangalia hatma ya wenzao, lakini
waligundulika kuwa nao walishiriki na baada ya kuwakamata na kuwahoji
wamekiri kuhusika na wao ndiyo walikimbia,” alisema.