WATU WATATU WAFARIKI SINGIDA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/watu-watatu-wafariki-singida.html
WATU watatu akiwemo Mkuu wa shule ya sekondari ya kata ya Ngimu,katika Halmashauri ya wilaya ya Singida wamekufa na wengine kumi kujeruhiwa kufuatia gari dogo aina ya Noah walilokuwa wakisafiria kutoka Kijiji cha Ngimu kuacha njia na kupinduka katika Kijiji cha Ijanuka,Manispaa ya Singida.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida,Dk.Deogratius Banuba amewataja waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na Mkuu wa shule ya sekondari ya kata ya Ngimu,Bibi Tatu Bunku mwenye umri wa kati ya miaka 45 na 50 aliyefia Hospitali ya Mkoa Singida wakati akipatiwa matibabu,
Wengine ni dereva wa gari hilo,Bwana Enock Edward Mbaga (31) mkazi wa Arusha na Bi Hajira Juma Ikhala (21)mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Ngumbu,Mkoani Shinyanga,ambaye alifariki papo hapo.
Aidha kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi huyo amesema kuwa jumla ya watu kumi wamelazwa kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida,Mrakibu Mwandamizi wa polisi,(SSP),Claud Kanyorota amesema tukio hilo limetokea leo saa moja asubuhi katika eneo la Kijiji cha Ijanuka,kata ya Kisasida,Manispaa ya Singida na amelitaja gari lililopata ajali hiyo kuwa ni lenye namba za usajili T.227 BLN Toyota Noah.
Aidha Kaimu kamanda huyo amesema kuwa uchunguzi wa awali wa polisi unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari hilo uliosababisha tairi la gari hiyo iliyokuwa na abiria 13 kupasuka na hivyo kupinduka na kisha kusababisha madhara hayo.
