Misri yawahukumu waandishi miaka 7 jela
Hatua ya mahakama ya Misri kuwakuta na hatia waandishi wa habari wa shirika la Al-Jazeera umelaaniwa na pande mbali mbali dunia, na nchi...
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/misri-yawahukumu-waandishi-miaka-7-jela.html
Hatua ya mahakama ya Misri kuwakuta na hatia waandishi wa habari wa
shirika la Al-Jazeera umelaaniwa na pande mbali mbali dunia, na nchi
kadhaa zimewaita mabalozi wa Misri kulalamikia uamuzi huo wa mahakama.
Ni sauti ya jaji wa mahakama mjini Cairo, akitangaza hukumu dhidi ya a
hao wa al-Jazeera,ambao ni pamoja na Peter Greste ambaye ni raia wa
Australia, Mohamed Fahmy raia wa Canada mwenye asili ya Misri, na Baher
Mohammed ambaye ni raia wa Misri. Mahakama hiyo imesema waandishi hao
wamekutwa na hatia katika mashitaka yenye uhusiano na ugaidi.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya waandishi wa habari ambao
hawakuwepo mahakamani, wamehukumiwa miaka 10 jela kila mmoja.Uamuzi huo ambao umepitishwa asubuhi ya leo umezusha laana kutoka pande mbali mbali, na hofu kuhusu hatima ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Misri. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Australia Julie Bishop amesema uamuzi huo umeishitua serikali ya nchi yake.
''Hukumu kama hii, haiendani na madai ya Misri kwamba iko katika kipindi cha mpito kuelekea demokrasia. Serikali ya Australia inaitaka serikali mpya ya Misri, kutafakari ujumbe ambao dunia inaupata juu ya hali ya mambo nchini humo, kupitia hukumu hii.'' Amesema bi Bishop.
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Australia amesema serikali yake inashindwa kuelewa kama kweli uamuzi huo umefikiwa kutokana na ushahidi ulioonyeshwa mahakamani.
Hukumu ya kuchukiza
Sio Australia pekee iliyokasirishwa na uamuzi huo wa mahakama ya Misri. Uingereza imesema imemuita balozi wa Misri nchini humo kulalamikia uamuzi huo ambao imeuita wa kuchukiza.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague, amesema amechukizwa kwa namna ya pekee na hitilafu zilizojitokeza wakati wa uendeshaji wa kesi dhidi ya waandishi hao, hususan upande wa mwendeshamashitaka kukataa kuonyesha ushahidi muhimu kwa upande wa utetezi.
Uholanzi ambayo mmoja wa waandishi waliohukumiwa bila kuwepo mahakamani ni raia wake, imemwita pia balozi wa Misri nchini humo, na waziri wa mambo ya nchi za nje Frans Timmermans amesema atalijadili suala hilo na mawaziri wenzake wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya katika mkutano unaofanyika Luxembourg.
Mchezo wa kuigiza mahakamani
Shirika la Amnesty International limesema hukumu dhidi ya waandishi hao ni kiza kwa uhuru wa kujieleza nchini MisriWaandishi wote wanaohusika katika kesi hiyo walituhumiwa kulisaidia kundi la Udugu wa Kiislamu lililopigwa marufuku, na kuichafua sura ya Misri baada kuondolewa madarakani rais kutoka kundi hilo, Mohammed Mursi.
Hukumu hiyo imetolewa siku moja baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry,ambaye akiwa mjini Cairo jana aliitolea wito Misri kuheshimu uhuru wa watu kutoa mawazo yao.
