Magoli mengi yafungwa katika hatua ya makundi
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/magoli-mengi-yafungwa-katika-hatua-ya.html
Ni wazi kuwa wachezaji mahiri wa soka ulimwenguni walibeba njumu zao za
kufunga magoli wakati wakielekea Brazil kwa Kombe la Dunia. Jumla ya
magoli 136 yametiwa kimyani katika mechi 48 za awamu ya makundi
Washindani 32 wa Kombe la Dunia walifunga karibu magoli matatu katika kila mchezo kwa kiwango cha wastani katika duru ya kwanza, ikilinganishwa na kiasi cha chini ya magoli mawili kwa kila mchezo (jumla ya 93) katika awamu hiyo nchini Afrika Kusini miaka minne iliyopita.
Rekodi za ufungaji mabao zimevunjwa. Algeria ndio timu ya kwanza ya Afrika kufunga manne, Asamoah Gyan ndiye mfungaji bora barani Afrika kwa kufunga magolo sita katika Kombe la Dunia, wakati Miroslav Klose wa Ujerumani ametoshana na Ronaldo wa Brazil kwa kufunga magoli 15.
Lakini juhudi za Klose kujaribu kuipiku rekodi ya Ronaldo huenda ikawa kibarua kigumu, ukilinganisha na kiwango cha mwenzake chipukizi Thomas Müller. Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye alifunga goli la ushindi dhidi ya Ujerumani, na mabao matatu dhidi ya Ureno, ana magoli tisa ya Kombe la Dunia. Müller hivyo basi alimpiku Diego Maradona wa Argentina na Mjerumani mwenzake Rudi Völler katika mechi ya Alhamisi.
Lionel Messi, Neymar na Arjen Robben ambao wanatamba sana katika timu za Argentina, Brazil na Uholanzi, wamezibeba timu zao kwa kufunga magoli manne kila mmoja. Xherdan Shaqiri wa Uswisi, Robin Van Persi wa Uholanzi, James Rodriguez wa Colombia wana matatu kila mmoja na wana kila dalili za kuendelea kutikisa nyavu za wapinzani.
Na dimba hili kufikia sasa halijakosa kuwashangaza wengi na nampisha mwenzangu Anuary Mkama akueleze namna ambavyo vigogo wa Ulaya walivyofunga virago vyao mapema kuelekea makwao baada ya majahazi yao kuzama..
