Flatnews

KWA HILI MARCIO MAXIMO UMETISHA, KIROHO SAFI! MAISHA YANATAKIWA KUENDELEA YANGA SC


http://api.ning.com/files/3QWN5yhdbad*V5J9Z5LXoyU9C1YTVF3ARcS-ZlArd17Iw3owr1m*DmjHowRQr048ZJABB9cF9ukZtJYjbfuCqnv0TYZxfQrl/maximo3.jpg
Mbrazil Marcio Maximo hakuwa na mahusiano mazuri na Juma Kaseja mwaka 2007 alipokuwa anaifundisha Taifa Stars, lakini sasa amesema kazi inatakiwa kundelea Yanga kama kawaida na kusahau yaliyopita


KOCHA Mbrazil, Marcio Maximo na msaidizi wake Leonadro Neiva wanatarajia kuanza kazi rasmi jumatatu baada ya kumwanga wino kuitumika Yanga sc  kwa mkataba wa miaka miwili.
Jana Maximo na mwenzake Neiva walikuwa na mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya Yanga, makutano ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es salaam ambapo walieleza malengo yao na kujibu maswali ya wanahabari.
Ulikuwa mkutano mzuri na muhimu kwa wanamichezo, kwasababu walikuwa na kiu ya kujua nini Maximo ataongea kwa mara ya kwanza baada ya kurudi nchini, safari hii ikiwa ni Yanga na sio majukumu ya kitaifa.
Moja ya mambo aliyosema Maximo ni kufurahia kurudi Tanzania, iliwasifu watanzania kwa kuwa wakarimu, wapenda mpira na akaahidi kufanya kazi kwa ueledi mkubwa.
Pili Maximo hakusita kutoa shukurani zake kwa viongozi wa Yanga kwasababu wamemuamini na kumpa nafasi hiyo muhimu. Alikiri kufuatwa kwa awamu tatu mfufulizo, lakini safari hii akaona bora akubali.
Kitu ambacho wengi walisubiri kusikia kutoka kwa Mbrazil huyu mwenye heshima kubwa nchini, nikiwemo mimi, ni mipango yake ya kuifanya Yanga kuwa bora.
Maximo alipata fursa ya kueleza mipango yake ambapo alisema anatarajia kuanza kazi moja kwa moja siku ya jumatatu pamoja na msaidizi wake Neiva kwa kushirikiana na kocha wa kikosi cha U-20.
Alisema ataanza na wachezaji waliopo na wachezaji wa kikosi cha U20 ambapo watakua wakifanya mazoezi pamoja.
“Natambua tuna wachezaji wengi katika timu za Taifa mbalimbali ikiwemo ya Tanzania (Taifa Stars), Uganda  (The Cranes) na Rwanda (Amavubi) ambao wapo wanayatumikia mataifa yao, na punde watakapomaliza majukumu hayo wataungana nasi kwa maandalizi”.
 http://api.ning.com/files/u325ipbpd7ozI9RHanCNUNG8t3dlmbJCQrftURfADlJojiZrB4L0yi0xSXmfHAtJAe6x5aVlP-4YQh1TqMXq9QPJHDvqjjV*/KasejaJuma.jpg
Juma Kaseja ataendelea kufanya kazi na Maximo
Alisema mambo mengi, lakini yote yalilenga kuijenga Yanga mpya. Hakusahau kuomba uvumilivu kwa wanachama na mashabiki wa Yanga kwasababu soka linahitaji kwenda kwa namna mbili.
Moja unaweza kwenda haraka na mipango, lakini njia bora kwa klabu kama Yanga ni kwenda taratibu kwasababu ina safari ndefu ya kufikia kilele cha mafanikio.
Maneno ya Maximo yanaenda sambamba na kocha aliyekuwa anaifundisha Taifa stars kabla ya Mart Nooij, Mdenish Kim Poulsen.
Mara nyingi Kim alikuwa anapenda kusema “Things Takes Time” (TTT) . Kwa tafsiri isiyo rasmi, anamaanisha mambo yanahitaji muda.
Kila jambo linahitaji kupewa muda ili lifanyike vizuri. Walimu wengi wa soka wanajua hili, soka si jambo la haraka. Hata hao wanaoonekana kuwa bora duniani, walitumia muda mrefu kujenga soka lao.
Yanga ni klabu kongwe kiumri, lakini kimafanikio, hasa ngazi ya kimataifa ni changa. Mipango thabiti inatakiwa kuwekwa, lakini lazima uvumilivu uwepo.
Maximo ni mtu wa mipango, ni muumini wa falsafa yake, ana namna ya kufanya mambo yake, ana msimamo mkali hasa masuala ya nidhamu, hivyo wanachama, viongozi na wadau wa Yanga wamuamini na kumuacha atekeleze mipango yake ili siku moja Yanga ifike mbali.
Lakini yote kwa yote, Maximo alisema mambo mengi muhimu. Kuna watu walisubiri kuuliza maswali, na moja ya swali nililotegemea kulisikia jana ni kuhusu Juma Kaseja.
Kaseja ni kipa mkongwe, na wengi wanamuita `Tanzania One`. Kwa miaka takribani 10 aliichezea Simba kwa mafanikio.
Alifanya kazi nzuri medani ya kitaifa na kimataifa, lakini baadaye viongozi wa Simba walimtoa kafara na kushindwa kabisa kumuheshimu.
Yalisemwa mengi lakini sababu waliyosema viongozi ni kwamba kipa huyo alikuwa ameshuka kiwango.
 KASEJA6
Juma Kaseja alifungwa bao rahisi na Awadh Juma katika mechi ya Nani Mtani jembe, mwezi desemba mwaka jana, lakini ilikuwa sehemu ya mchezo. Picha kwa hisani ya Global Publisher.
Kaseja baada ya kumaliza mkataba wake na Simba msimu wa 2012/2013, hakuongezewa, na alilazimika kukaa nusu msimu (2013/2014) baada ya kukosa timu.
Yanga waliokuwa na majukumu ya ligi ya mabingwa barani Afrika, walilazimika kumsajili Kaseja mwenye uzoefu.
 Usajili huo ulizua mengi, lakini mwisho wa siku, viongozi wa Jangwani walisema uzoefu wa Kaseja ndio umewavutia kumsainisha na atatumika katika michuano ya kimataifa.
Wakati Kaseja akisajiliwa kwenda Yanga, nilihofia atapata matatizo kutokana na hali halisi iliyokuwa imemtokea nyuma na klabu yake ya Simba.
Kitendo cha kuachwa na kushindwa kuheshimika, kilimvuruga Kaseja na kila ukikutana naye alikuwa anaonekana mwenye mawazo.
Kwa kazi aliyofanya Simba, sidhani kama alitarajia kuachwa kwa namna ile. Haikuwa haki, ingawa Simba walikuwa na chaguo lao. Hakuna ambaye angeweza kuwalazimisha kumbakisha kipa huyu aliyewasaidia kuitoa Zamalek, ligi ya mabingwa mwaka 2003.
Baada ya kurudi Yanga kwa mara ya pili Kaseja aliidakia klabu hiyo kwenye mechi ya `Nani Mtani Jembe`. Hii ilikuwa mwezi desemba mwaka jana uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
Baada ya kuona kikosi cha kwanza kilichopangwa na aliyekuwa kocha mkuu, Mholanzi, Ernie Brandts akisaidiwa na Fredy Felix Minziro, niligundua kuwepo kwa majina mawili muhimu, Juma Kaseja na Emmanuel Okwi.
Hawa walisubiriwa sana siku hiyo. Yanga walifungwa mabao 3-1, huku bao la kufutia machozi likifungwa na Okwi aliyekuwa gumzo kwa wakati huo.
Kwa bahati mbaya sana, Kaseja alifanya kosa moja kubwa lililosababisha kufungwa goli la kizembe na mshambuliaji wa Simba, Awadh Juma.
Hili lilikuwa bao jepesi na kwa vyovyote vile Kaseja alilazimika kubeba lawama.
Wakati natoka uwanjani, nilipita jukwaa la Yanga, hakika mashabiki waliowengi walilaumu na wengine kusema Kaseja hana lolote.
Kimpira, kosa la Kaseja lilikuwa la kawaida, hata akina Iker Casillas wanafungwa mabao kama yake. Si mliona kombe la dunia Casillas akifanya makosa?
Baada ya tukio lile, ilionekana wanachama na wapenzi wengi wa Yanga wanakosa imani na Kaseja. Kama kawaida ya Watanzania, wachezaji wanabeba lawama kubwa wanapofanya makosa uwanjani.
Wengi wanasahau kuwa mpira ni mchezo wa makosa. Ili ufunge bao lazima mpinzani wako afanye kosa. Wapi uliona goli linafungwa bila kufanyika kosa? Yatakuwa maajabu.
Kila goli ni matokeo ya makosa. Kukosea kwa Kaseja ilikuwa kawaida na ni mambo ya mpira.  kaseja
Kaseja akiwa kazini Yanga sc
Lakini alipoanza kuichezea Yanga kwenye michuano ya ligi kuu mzunguko wa pili msimu uliopita, kwa bahati mbaya sana, Kaseja alifanya kosa mwezi machi mwaka huu kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ndani ya uwanja wa Jamhuri kwa kufungwa bao jepesi na mechi kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mechi hii ilikuja siku chache baada ya Yanga kutolewa kwa mikwaju ya penati na National Al Ahly ya Misri katika michuano ya ligi ya mabingwa.
Kaseja alianza katika mechi hii baada ya kipa namba moja, Deo Munish kukatwa mkono wake na bati akiwa nyumbani kwake.
Baada ya mchezo huo, Kaseja akaendelea kutupiwa lawama, na alipoenda Tanga kucheza dhidi ya Mgambo ambapo Yanga walifungwa 2-1 na kuanza kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa, alifungwa bao jepesi kwa mara nyingine.
Mambo yakawa mabaya zaidi, presha kubwa ya mashabiki wa Yanga ilimfanya kaseja apoteze hali ya kujiamini.
Nakumbuka kwenye mchezo wa Azam dhidi ya Yanga uwanja wa Taifa ambapo timu hizo zilitoka sare ya 1-1, Kaseja alicheza kwa wasiwasi mkubwa.
Lakini haya yalitokea kwa Kaseja kama yanavyotokea kwa makipa wengine bora duniani. Tatizo la mashabiki wengi wa Tanzania wanaangalia mpira wa ulaya kwa jicho lingine na mpira wa Tanzania.
Ulaya wachezaji wanakosea na mashabiki wa Tanzania wanaona ni kawaida, lakini kwetu mtu akifanya kosa kama la Casillas, basi utasikia kauza mechi, kahujumu…na maneno mengi.
Katika historia ya Kaseja, kamwe hakuwahi kuwa na uhusiano mzuri na kocha Maximo wakati huo akiifundisha Taifa stars. Kaseja alikuwa na tatizo na Maximo mwaka 2007, na nadhani lilianzia katika kipigo cha 4-0 kutoka kwa Senegal mjini Dakar.
Inasemekana Kaseja aligoma kumbadili Ivo Mapunda aliyekuwa amefungwa bao 4-0 kwa muda mfupi wa kipindi cha pili.
Tangu hapo Kaseja hakuwahi kuichezea Taifa stars chini ya Maximo. Watu walishinikiza kuitwa kwa Kaseja, lakini kama nilivyosema, Maximo ni mtu wa msimamo mkali na anapenda kufanya mambo yake kwa namna yake.
Jana wengi walitamani kusikia kauli ya Maximo kuhusu Kaseja ambaye anakutana naye Yanga sc. Wawili hawa wanakwenda kufanya kazi pamoja.
Maximo aliulizwa swali kuhusu Kaseja ambapo alikiri kuwa waliwahi kuwa na matatizo, lakini yale yalishapita.
“Najua ni kipa mzuri mwenye uwezo na uzoefu wa kutosha na kipindi hiki najivunia kuwa na makipa watatu wenye uwezo mzuri. Yaliyopita yameshapita,  yalikuwa ni timu ya Taifa na sasa tumekutana Yanga. kazi yetu ni moja tu kuifanya klabu iwe kwenye hadhi ya Kimataifa zaidi”.
Kauli hii ilionesha ukomavu wa Maximo. Kipindi kile ilikuwa timu ya Taifa, lakini sasa wanaungana Yanga kufanya kazi moja ya kuisaidia klabu.
Kwa maisha ya wengi ni ngumu kufanya kazi na mtu mliyekuwa naye na `bifu` na hii inatokana na kuendekeza chuki za ajabu.
Kama mlikuwa na `bifu` na mtu mkiwa Yanga, kwanini muendeleze `bifu` mkikutana Simba au Azam fc?
Kibongo bongo inawezekana kwasababu wengi hawana nidhamu na kujali kazi. Maximo anaamini Kaseja anaweza kumsaidia. Hawezi kukumbuka ya Taifa stars akiwa Yanga.
Huu ni mtazamo sahihi na naamini wanachama na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kumsapoti Maximo ili Kaseja arejee kwenye kiwango chake.
Bado ni kijana, ana miaka 29. Kaseja ana miaka mingi ya kucheza mbeleni, lazima aaminiwe.
Bahati nzuri viongozi wa Yanga wametambua haraka na kumuacha aendelee kuichezea timu hiyo msimu ujao. Naamini Kaseja atafanya kazi nzuri akiaminiwa.
Mashabiki punguzeni presha juu yake, mnamharibia ufanisi wa kazi.
Kuwa na makipa watatu wenye uzoefu, Juma Kaseja, Deo Munish `Dida` na Ally Mustafa `Barthez` ni faida kwa klabu. Waacheni wachuane katika mazoezi ya kocha wa makipa, Juma Pondamali `Mensah` na mwenye kiwango ataanza chini ya Maximo.

Post a Comment

emo-but-icon

item