Flatnews

HAWA NDIO WACHEZAJI 32 WANAOTARAJIWA KUNG'ARA ZAIDI NA KUONGOZA TIMU ZAO WAKATI WA FIFA WORLD CUP 2014


fifa world cup 2014

Fainali za Kombe la Dunia ni uwanja mpana. Ni mahali ambapo vipaji na vipaji vya wanasoka duniani huonekana. Madalali wa kuvumbua na kununua wachezaji [scouts] hufurika kwenye mashindano kama haya wakijua wazi kabisa kwamba pale ndipo watakapoona “lulu” kwa ajili ya vilabu vyao. Kwa maana hiyo kuna kila aina ya harakati za kimichezo na kuonyesha na kuonyeshana vipaji. Hii sio kumaanisha kwamba wachezaji wote mahiri hapa duniani walicheza katika fainali za Kombe la Dunia.La. Wapo wasakata kabumbu kadhaa ambao hawakuwahi kugusa fainali hizi.Mfano ni George Opong Weah na watu kama kina George West nk.

Lakini wakati wengine wakionyesha vipaji ili wang’amuliwe na kubadilisha maisha yao ya kisoka,wapo wale ambao wanashuka dimbani tayari wakiwa na majina [superstars] na ambao dunia tayari inakuwa ikiwaangalia kwa makini kutaka kujua na kuona kile watakachokifanya. Kila timu huwa na mchezaji ambaye hutizamwa zaidi. Kwa umombo unaweza kumuita Key Player. Kila timu,kwa kupenda au kutopenda,huwa ina star player. Hii haimanishi kwamba katika timu hakuna wachezaji wengine wenye majina au wanaoweza pia kuwa stars.La. Ni sheria ya mmoja mmoja inayozingatiwa hapa.
Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa soka,wachezaji hawa 32 [mmoja kutoka katika kila timu inayoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu] ndio watarajiwa kuchomoza zaidi huko Brazil. Mpangilio huu hapa ni kutokana na makundi ya FIFA World Cup 2014. NB: Orodha hii inaweza kubadilika kwani imeandikwa kabla timu zote hazijathibitisha wachezaji wake 23 iliyowachagua mwisho. Wengine wanaweza kuumia katika siku hizi za mwisho na hivyo kutokwenda Brazil.Zingatia.

Neymar-Brazil.
Neymar-Brazil.
Hakuna ubishi kwamba Neymar anayechezea soka la kulipwa Barcelona nchini Spain ndio gumzo kubwa kwa timu ya Brazil. Anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya The Kings Of Samba[Brazil]
Oribe Peralta-Mexico
Oribe Peralta-Mexico
Ingawa wachezaji wengine wa Mexico kama Chicharito na Giovani dos Santos wanatajwa kama ma-star,Oribe Peralta ambaye anacheza katika ligi ya nyumbani katika club ya Santos Laguna, ndiye anaaminika hivi sasa kuwa star zaidi
Luka Modric-Croatia
Luka Modric-Croatia
Hakuna shaka kwamba Luka Modric ndiye mchezaji star zaidi hivi sasa katika timu ya Croatia. Kiungo huyu ambaye hivi sasa anachezea timu ya Real Madrid nchini Spain ameonekana wazi kuwa tegemeo sio tu katika club bali nchi yake Croatia.
Charles Itandje-Cameroon
Charles Itandje-Cameroon
Ingawa ungetegemea mchezaji kama Samuel E’too kuendelea kuwa star na tegemeo zaidi katika timu ya Cameroon, golikipa Charles Itandje ndio tegemeo na ambaye wengi watapenda kumuona akiokoa mikwaji. Charles ambaye anachezea timu ya Konyaspor nchini Uturuki[kwa mkopo kutoka PAOK FC ya Ugiriki] aling’ara vilivyo katika mchezo dhidi ya Tunisia wakati wa kuwania nafasi ya kwenda Brazil.Google utaona alichofanya.
Diego Costa-Spain
Diego Costa-Spain
Ingawa bado kuna utata kuhusu hali yake na kama atakuwa fit kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia huko Brazil,Diego Costa mshambuliaji mahiri wa timu ya Atletico Madrid anatarajiwa kuwa nyota wa Spain. Lakini pia huenda akawa ndiye mchezaji atakayezomewa zaidi huko Brazil kwani Diego ni mzaliwa wa Brazil na angeweza kabisa kuchezea Brazil mwaka huu kama asingeamua kuchezea Spain[pia ni raia wa Spain].Wabrazil hawajaipenda hiyo.
Arjen Robben-Holland[The Netherlands]
Arjen Robben-Holland[The Netherlands]
Robben,mshambuliaji mahiri ambaye hivi sasa anaendelea kuwika na timu ya Bayern Munich nchini Ujerumani,ndiye mchezaji ambaye ni star zaidi na ambaye ameonyesha kuwa na kile kiwango kinachoitwa “cha dunia”. Ana miaka 30 hivi sasa.
Arturo Vidal-Chile
Arturo Vidal-Chile
Arturo ambaye anachezea club ya Juventus nchini Italia ni mchezaji “kiraka” wa Chile ambaye endapo Chile itaushangaza ulimwengu wa soka huko Brazil,bila shaka mchango wake utakuwa mkubwa.
Tim Cahill-Australia
Tim Cahill-Australia
Tim Cahill anayechezea timu ya New York Red Bulls katika ligi ya soka ya Marekani na Canada[Thiery Henry alipitia hapo baada ya Ulaya] ndiye nyota kwa upande wa Australia.
James Rodriguez “Hames”-Colombia
James Rodriguez “Hames”-Colombia
Kwa upande wa Colombia Ramadel Falcao, ndio mchezaji nyota zaidi.Lakini kuna kila aina ya dalili kwamba mwaka huu hatoweza kucheza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.Hapo ndipo James Rodriguez anapochukua nafasi. Rodriguez au Hames kama anavyoitwa na mashabiki wa soka huko Colombia, anachezea AS Monaco ya Ufaransa.
Yaya Toure-Ivory Coast
Yaya Toure-Ivory Coast
Kama yupo mchezaji kutoka barani Afrika[bila kujali timu] ambaye sio tu anapendwa na mashabiki wengi barani Afrika hivi na ambaye yupo kwenye kiwango cha juu,basi bila shaka ni Yaya Toure. Hata wachezaji wenzake wa Ivory Coast kama vile mkongwe Didier Drogba,wote wanamtaja Yaya kuwa kiongozi na mhimili wa timu yao. Yaya anachezea mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, EPL Champions, Manchester City
Kostas Mitroglou-Greece
Kostas Mitroglou-Greece
Ingawa mashabiki wa Ligi Kuu ya Uingereza bado hawajapata nafasi ya kuona vizuri makeke ya Kostas ambaye anacheza katika klabu ya Fulham, ni wazi kwamba yeye ndio tegemeo kubwa la timu ya Ugiriki katika mashindano ya mwaka huu.
Keisuke Honda-Japan
Keisuke Honda-Japan
Ingawa Japan wanao mastar wengine kama vile Shinji Kagawa anayechezea Manchester United,hakuna ubishi kwamba Keisuke Honda ndiye mhimili mkuu kwa sasa. Anachezea AC Milan nchini Italy.
Wayne Rooney-England
Wayne Rooney-England
Ingawa msimu wa ligi kwa upande wa timu yake ya Manchester United haukuwa wa kuvutia sana, Wayne Rooney au ukipenda unaweza kumuita Wazza anabakia kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo zaidi kwa upande wa timu ya taifa ya Uingereza. Hana historia nzuri sana na mashindano ya Kombe La Dunia lakini endapo kelele za waingereza[na wana kelele kweli] zitakuwepo,basi Wazza anaweza kuwa chanzo.
Mario Balotelli-Italy
Mario Balotelli-Italy
Miaka kadhaa iliyopita[na hata hivi sasa miongoni mwa watu] ni vigumu kuamini kwamba mtu mweusi ndio key player kwa timu ya taifa ya Italy. Muda umebadilika na mchezaji huyu mwenye mbwembwe,hasira na kila aina ya vituko ndiye ataangaliwa zaidi pindi timu yake ya Azzurii itakapoteremka dimbani huko Brazil.
Luis Suarez-Uruguay
Luis Suarez-Uruguay
Kama ilivyo kwa Balotelli hapo juu,Luis Suarez ni mchezaji mwingine ambaye ana kila aina ya vioja. Pamoja na hayo ni mfungaji hodari na ndio tegemeo kubwa la Uruguay huko Brazil.Kwa bahati nzuri au mbaya,Uruguay wapo kundi moja England na hivyo lazima watapimana joto. Upinzani kutoka Liverpool utaendelea?Tutaona.
Keylor Navas-Costa Rica
Keylor Navas-Costa Rica
Sio mara nyingi sana kuwemo kwenye Kombe la Dunia na kisha kutamba kwamba mchezaji wenu mhimili ni kipa.Costa Rica wao wanaweza kusema hivyo kwani Keylor Navas anayechezea timu ya Levante nchini Spain ndio mhimili na ambaye anategemewa kulinda mlango na kuongoza wenzake.
Franck Ribery-France
Franck Ribery-France
Ukisema Franck Ribery wa Bayern Munich basi bila shaka itabidi pia useme Franck Ribery wa Ufaransa. Ndio tegemeo. Mwaka huu alikuwepo katika wachezaji watatu wa juu waliokuwa wanawania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA.
Xherdan Shaqiri-Switzerland
Xherdan Shaqiri-Switzerland
Endapo Switzerland itakuwa na mafanikio makubwa huko Brazil,basi Xherdan ndio atakuwa mpishi mkuu.Anachezea Bayern Munich pembeni ya Ribery na Arjen Robben.
Antonio Valencia-Equador
Antonio Valencia-Equador
Winga huyu ambaye anachezea Manchester United ndio tegemeo kubwa la Equador katika mashindano ya mwaka huu.Wenzake wanamuita “kiongozi”.
Emilio Izaguirre-Honduras
Emilio Izaguirre-Honduras
Emilio anachezea Celtic FC kule Uskochi. Kwa upande wa Honduras ndiye tegemeo kubwa hususani kwa upande wa ulinzi na kusukuma mbele mashambulizi.
Lionel Messi-Argentina
Lionel Messi-Argentina
Hakuna ubishi kwamba Messi ni miongoni mwa wachezaji mahiri kabisa waliowahi kuucheza mchezo wa soka hapa duniani.Hata hivyo, ana kasoro moja kwa mujibu wa wachambuzi wa soka na hususani wasiompenda;hajawahi kushinda Kombe La Dunia. Kwa maana hiyo,kama unadhani Neymar wa Brazil ana presha ya kuipa Brazil kombe,Messi pia anayo na zaidi.Argentina na ulimwengu unasubiri…ataiwezesha kushinda Kombe La Dunia mwaka huu?
Edin Dzeko-Bosnia & Herzegovina
Edin Dzeko-Bosnia & Herzegovina
Bosnia & Herzegovina ni wageni katika fainali za Kombe La Dunia.Hii ndio mara yao ya kwanza. Pamoja na hayo,wanaye Edin Dzeko mshambuliaji anayechezea mabingwa wa Uingereza,Manchester City. Ndiye atagemewa kuwaongoza wenzake kufanya “muujiza” huko Brazil.
Ashkan Dejagah-Iran
Ashkan Dejagah-Iran
Iran wanasema hawaendi Brazil “kutalii”.Bila shaka wanasema hivyo wakiangalia wachezaji wao kama Ashkan Dejagah ambaye anacheza soka ya kulipwa nchini Uingereza. Huyu bwana anao pia uraia wa Ujerumani na alipokuwa mdogo aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Ujerumani akiwa na Mesut Ozil.
Emmanuel Emenike-Nigeria
Emmanuel Emenike-Nigeria
Ingawa ligi anayochezea[Uturuki] haina umaarufu sana, hakuna ambaye anatilia shaka uwezo wa Emmanuel Emenike katika soka. Ni mshambuliaji mahiri na makini. Anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya Nigeria[Super Eagles] timu ambayo inatarajiwa kufanya vizuri huko Brazil.
Phillip Lahm-Germany
Phillip Lahm-Germany
Miongoni mwa wachezaji wa timu ya Ujerumani ambao ni vigumu sana kwa kocha wa Ujerumani,Joachim Low, kupata mtu wa kuziba pengo lake[endapo itatokea akaumia au vinginevyo] ni Kapteni Phillip Lahm. Mchezaji huyu ambaye anachezea Bayern Munich ni muhimu na ndiye anaongoza Ujerumani huko Brazil ikitarajiwa kwamba mwaka huu watafanya vyema zaidi.
Majeed Waris-Ghana
Majeed Waris-Ghana
Ghana au Black Star ni miongoni mwa timu kutoka Africa ambazo zinatarajiwa kufanya vyema nchini Brazil. Kama utakumbuka,Ghana katika fainali za Afrika Kusini mwaka 2010 walibakia almanusura kutoboa na kufika nusu fainali. Majeed Waris anayechezea soka la kulipwa FC Valenticiennes huko Ufaransa anajua vyema wakati gani apige,akimbie nk.Ni mchezaji ambaye anatarajiwa kuipa forwardline ya Ghana uhai mkubwa na kushirikiana vyema na Asamoah Gyan.
Clint Dempsey- USA
Clint Dempsey- USA
Hakuna ubishi kwamba mchezaji wa US ambaye alikuwa anatizamwa na wengi kuongoza timu ya nchi hiyo ni London Donovan. Kwa bahati mbaya kocha mjerumani Jurgen Klinsman, hakuona hivyo. Donovan katemwa. Badala yake mchezaji Clint Dempsey ndiye ambaye anatarajiwa kuongoza jahali za USA.
Christiano Ronaldo-Portugal
Christiano Ronaldo-Portugal
Hivi sasa ndiye anashikilia taji la FIFA La Mchezaji Bora wa Dunia. Timu anayochezea,Real Madrid ndio mabingwa wa Ulaya na yeye akiwa na rekodi ya magoli 17 ya Ligi ya Mabingwa. Hakuna ubishi kwamba Portugal wanakwenda Brazil kutokana na mchango wake mkubwa hususani katika ile mechi iliyowaweka pembeni Sweden. Ronaldo au CR7 ndiye mhimili mkubwa wa Ureno.
Eden Hazard-Belgium
Eden Hazard-Belgium
Swahiba wangu wa karibu,Esmail Manambi,majuzi alinikumbusha kwamba Ubelgiji,ingawa sio miongoni mwa timu zinazotajwa sana linapozungumziwa suala la Ubingwa wa Dunia, wanaweza kuushangaza ulimwengu. Nakubaliana naye kabisa. Ubelgiji ya mwaka huu imejaa wachezaji wenye vipaji na majina. Kuna kila Kompany,Lukaku,Fellaini nk. Wote,hata hivyo,wanaangalia zaidi kwa Eden Hazard ambaye mwaka jana Chelsea walikohoa paundi Milioni 32 kumnunua.
Roman Shirokov-Russia
Roman Shirokov-Russia
Kama utakumbuka wakati wa fainali za South Africa kocha wa Uingereza wakati huo,Fabio Capello kidogo apate wazimu.Ule utulivu wake uliisha ghafla. Wanasema kelele za Vuvuzela zilizingua sana. Hivi sasa Capello ndio kocha wa Urusi. Na kama kuna mchezaji ambaye anaweza kusaidia kutorudisha ule mzimu wa Capello South Africa basi mchezaji huyo ni Roman Shirokov anayechezea Krasnodar.Ndiye Kapteni wa Urusi.
Roman Shirokov-Russia
Ki Sung-Yueng-South Korea
Ingawa Korea Kusini inapewa nafasi ndogo zaidi kunako Ubelgiji na Urusi katika kundi lao, endapo watasonga mbele basi bila shaka mchango wa Ki Sung Yueng anayechezea Sunderland kwa mkopo kutoka Swansea,hautokuwa mdogo.Ndiye tegemeo kubwa la Korea ya Kusini.
Madjid Bougherra-Algeria
Madjid Bougherra-Algeria

Algeria ni timu nyingine kutoka Afrika mwaka huu.Nchi hii ina uzoefu zaidi wa Kombe la Dunia. Kapteni wao Madjid Bougherra anayecheza soka lake la kulipwa nchini Qatar na timu ya Lekhwiya, ndiye anayetarajiwa kuongoza jahazi.Ameshachezea nchi yake katika zaidi ya mechi 60.

Post a Comment

emo-but-icon

item