Wanafunzi wa Mzumbe wafariki dunia kwenye bwawa la samaki
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,SACP Ahmed Msangi
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/wanafunzi-wa-mzumbe-wafariki-dunia.html

Mbeya.
Watu watatu wamefariki dunia wakiwamo wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, ambao walipoteza maisha baada ya kuzama
kwenye bwawa la samaki.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema jana kwamba wanafunzi
Michael Tarimo (20) na Albert Shenkalwa (23) walifariki dunia juzi baada
mtumbwi waliokuwa wakiutumia kupinduka kwenye bwawa maalumu la samaki
linalosimamiwa na Hospitali Teule ya Ifisi eneo la Mbalizi jijini hapa.
Msangi
alisema bwawa hilo ni sehemu ya ‘Zoo ya wanyama’ inayosimamiwa na
hospitali hiyo ambapo watu mbalimbali wanafanya utalii kutembelea na
kujionea wanyama wa aina mbalimbali pamoja na kupanda mtumbwi kwenye
bwawa dogo.
Alisema
wanafunzi hao walikuwa wakisomea stashahada ya biashara na kwamba
walikwenda huko pamoja na wenzao 12, kwenye ‘pikiniki.’ Alisema pamoja
na kuangalia wanyama pia walikwenda kwenye bwawa linalotunza samaki
ambako walipanda mtumbwi lakini ulijigeuza ghafla na walishindwa
kuogelea.
“Kwa
kawaida katika bwawa hilo, watu hawaruhusiwa kuogelea isipokuwa kuingia
kwa mtumbwi,’’ alisema. Kuhusu kifo cha mtu wa tatu, Kamanda Msangi
alisema mkazi wa Kijiji cha Mpolo-Igawa, wilayani Mbarali Anaheri Lazaro
(43) aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye kilabu cha pombe za
kienyeji. Msangi alisema uchunguzi wa polisi uligundua kwamba silaha
iliyotumika ni gobori baada ya kuokotwa golori moja eneo la tukio.
Alisema chanzo cha mauaji kinachunguzwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa Kituo cha Afya Igurusi.