WAANDISHI WA SHERIA MBIONI KUNOLEWA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/waandishi-wa-sheria-mbioni-kunolewa.html
WAANaibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki akiagana na
Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Maendeleo (UNDP) Bi. Mandisa Mashologu (kulia) alipomtembelea Naibu
Waziri ofisini kwake, Mtaa wa Mkwepu, jijini Dar es Salaam leo
(Jumatatu, Mei 19, 2014). Katikati ni Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw.
Philippe Poinsot. (Picha na Wizara ya katiba na Sheria)
Serikali
kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Maendeleo (UNDP) inatarajia kutoa mafunzo kwa Waandishi wa Sheria kwa
lengo la kuwaongezea uwezo wa kuandaa miswada katika lugha ya kiswahili –
lugha ambayo inatumiwa na watanzania wengi.
Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki amemwambia
Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Philippe Poinsot kuwa kwa sasa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatekeleza mkakati wa kuandaa miswada yote
inayosilishwa Bungeni katika lugha mbili, Kiingereza na Kiswahili ili
kuwawezesha wananchi wengi kuisoma.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, katika kutekeleza kazi hiyo,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Uandishi wa
Sheria inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa watumishi na
uwezo na hivyo kuhitaji msaada wa mafunzo.
“Kwa
sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina kazi ya kuandaa miswada katika lugha
mbili ikiwemo Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya taifa ambayo wananchi
wengi wanaifahamu,” alisema Bi. Kairuki katika mkutano wake na Bw.
Poinsot leo (Jumatatu, Mei 19, 2014) jijini Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulifanyika katika ofisi ya Naibu Waziri Kairuki jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George
Masaju, Mkurugenzi wa Mashtaka Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu
Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bi. Mandisa Mashologu na maafisa wengine
waandamizi wa serikali.
Akizungumza
katika mkutano huo, Bw. Masaju alisema kwa sasa Ofisi yake ina
Waandishi wa Sheria 18 tu na kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na
majukumu ya Idara ya Uandishi wa Sheria.
“Serikali
imeanzisha utaratibu huu wa kuandaa miswada katika lugha mbili lakini
tuna changamoto ya uhaba wa watumishi na hata hao waliopo, walifundishwa
kuandaa miswada katika lugha ya kiingereza na hivyo kuhitaji mafunzo,”
alisema Bw. Masaju.
Akiongea
katika mkutano huo, Bw. Poinsot alisema Shirika lake limepokea maombi
ya Serikali na kuwa litayafanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali ili
hatimaye miradi hiyo itekelezwe.
“Kwetu
sisi UNDP, sekta ya sheria ni muhimu sana hususan katika miradi
inayolenga kuwasaidia masikini na kujenga uwezo … ndiyo maana tupo
tayari kuisadia,” alisema kiongozi huyo wa UNDP hapa nchini.
Kwa
mujibu wa Bw. Poinsot, Shirika lake limepanga kuisaidia Serikali kupitia
mradi wake unaolenga kuimarisha usimamizi wa utoaji haki (Strengthening
Administartion of Justice Project). Miradi ya awali inatarajiwa kuanza
kutekelezewa hivi karibuni kabla ya kuanza kutekelezwa kwa awamu ya pili
ya Mpango Maalum wa Shirika hilo (UNDAP II) unaotarajia kuanza
kutekelezwa mwezi Januari 2015.
Maeneo
mengine ambayo Serikali na UNDP zinatarajia kushirikiana ni katika
utoaji wa huduma za msaada wa kisheria; kuimarisha uwezo wa waendesha
mashtaka na watumishi wa mahakama; na kuboresha mifumo ya uendeshaji ili
kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.