Flatnews

SIMULIZI YA RECHO INAUMA

HUKU   makovu ya machungu ya kifo cha msanii wa filamu za Kibongo, Rachel (Sheila) Leo Haule ‘Recho’ yakiwa bado hayajakauka, Risasi si l...


HUKU makovu ya machungu ya kifo cha msanii wa filamu za Kibongo, Rachel (Sheila) Leo Haule ‘Recho’ yakiwa bado hayajakauka, Risasi si linakupa simulizi yenye maumivu kuhusu marehemu huyo.
Mchumba wa marehemu Saguda akilia kwa uchungu.
Recho alifariki dunia Mei 27, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum ‘ICU’ baada ya kujifungua na mtoto kufariki dunia muda mfupi baadaye.
Staa huyo alijifungua kwa upasuaji mtoto wa kiume, lakini kwa bahati mbaya tatizo la presha ya kushuka na sukari lilimpata na hivyo kuanza kupatiwa huduma ya haraka kabla ya mauti kumkuta.
Recho alijifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi Lugalo, Jumapili Mei 25, mwaka huu na hali ilipobadilika alikimbizwa Muhimbili, kabla ya mauti kumfika.

SIMULIZI YENYEWE
Mchumba anayeonekana ni mume wa marehemu Recho, George Saguda ambaye uhusiano wao ni wa miaka takribani mitano sasa, alisimulia mazito kuhusu uhusiano wake na marehemu huyo.
Waombolezaji wakiwa kwenye mazishi.
Katika mazungumzo na gazeti hili, juzi Jumatano, Sinza – Palestina jijini Dar, nyumbani kwa mjomba wa marehemu Recho ambapo msiba uliwekwa, Saguda alisema kamwe hawezi kumsahau Recho.
“Nina machungu sana moyoni.
Naumia kumpoteza mke wangu na mwanangu. Walikuwa muhimu sana kwangu. Ndoto zote zimezimika. Ulikuwa mwanzo mzuri wa maisha yetu tuliyokuwa tumeyapanga,” alisema Saguda.
Akaongeza:
“Sikuwa na hili wala lile. Taarifa za kifo cha Recho bado kama ndoto, ningefurahi kama ingekuwa hivyo. Tulipanga mengi na Recho, sikujua kama mwisho wake ulikuwa umefika.”
SHOPPING YA MTOTO
“Tulijiandaa vizuri sana kumpokea mtoto wetu. Siku chache kabla ya kusikia uchungu, tulikwenda madukani kumfanyia mtoto shopping. Tulitumia zaidi ya shilingi laki nane (800,000).
“Tulimchagulia nguo nzuri na vitu vingine muhimu kwa ajili yake, kumbe Mungu alikuwa ameshapanga yake (analia).”
SIMANZI TUPU
“Tulimfikisha Recho salama Hospitali ya Lugalo, akajifungua vizuri mtoto wa kiume. Nakumbuka ilikuwa Jumapili usiku. Lakini kutokana na hali ya mtoto ilivyokuwa, hakupewa. Aliwekwa chini ya uangalizi wa manesi.
“Mke wangu hakuwa na hali mbaya ya kutisha, niliondoka hospitalini na tukawa tunatumiana meseji ule usiku. Ni picha ambayo inagoma kufutika kichwani mwangu.”
RECHO ALIMPONGEZA
“Kuna meseji alinitumia, akasema: Mume wangu nimekuzalia kidume, naona sasa utakuwa umepata mtu wa kwenda naye uwanjani kushangilia mpira, siku Yanga ikicheza.
“Meseji hiyo inaniumiza sana. Nashindwa kuamini kilichoendelea, moyo wangu una majonzi sana. Ni ngumu kukubali kifo kilichotokea usiku wa Jumatatu wakati Jumapili tu nilikuwa nachati naye. Sijielewielewi kwa kweli.”
WASIWASI
Anasema usiku wa Jumapili akiwa wodini, alimwangalia Recho na kuona namna hali yake ilivyobadilika, akamwambia: “Mke wangu naona kama hali yako siyo nzuri, umechoka sana lakini jikaze, utapata nafuu tu.”
Saguda anasema alipomwambia Recho hivyo, alimjibu kwa kujitahidi: “Usijali baba, nitakuwa sawa, si unajua namna ninavyokuwaga presha yangu?”
MIPANGO YA MAISHA
Akizidi kumzungumzia marehemu, Saguda alisema Recho alikuwa mwanamke sahihi katika maisha yake kwani walipanga mengi na walianza kutekeleza kwa msaada mkubwa wa mawazo yake.
“Alikuwa mwanamke mwenye akili sana. Recho si mfujaji wa fedha. Unaweza kuacha shilingi milioni kumi (10,000,000) ndani asipate tamaa ya kuziingiza kwenye matumizi ambayo hayakuwa kwenye mipango.
“Nikiwa na Recho tumefanikiwa kufungua kampuni yetu ya Sara Entertainment (Sara ni kifupisho cha majina yao. Sa – Saguda na Ra – Rachel) na mpaka anafariki dunia tulishauza sinema mbili; Vanessa na Fedheha, zote zimefanya vizuri sana.
Tulikuwa tupo kwenye mipango ya kuanza kurekodi filamu nyingine.
“Alikuwa mwanamke anayeangalia maendeleo zaidi, hakupenda sana starehe. Kuna wakati nilimwambia sasa tununue gari, akasema hapana, tujijenge kwanza ndipo tununue gari, tena yeye akasema inafaa tununue Noah (Toyota) ili litusaidie pia location (shughuli za kurekodi).
“Niliishi na Recho lakini nakiri ilikuwa bila ridhaa ya wazazi wake maana nilikuwa bado sijajitambulisha. Tulikubaliana akijifungua tu, ndipo niende kwa mjomba wake tukakamilishe taratibu zote tufunge ndoa. Yote hayo yameyeyuka (analia tena).”

Post a Comment

emo-but-icon

item