MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AANZA ZIARA YA KIKAZI NCHINI JAPAN
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/makamu-wa-rais-dkt-bilal-aanza-ziara-ya.html
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara, Uchumi na Viwanda wa
Japan, Toshimitsu Motegi, (wa kwanza kulia) wakati alipofika ofisini kwa
Waziri huyo kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake nchini Japan, leo
Mei 20, 2014. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Japan, Salome
Sijaona.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akibadilishana zawadi na Waziri wa Biashara, Uchumi na Viwanda wa Japan,
Toshimitsu Motegi, baada ya mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Waziri
huyo akiwa katika ziara yake nchini Japan, leo Mei 20, 2014.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya JETRO, Hiroyuki
Ishige, wakati walipokutana na kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake
nchini Japan, leo.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akibadilishana zawadi na Mwenyekiti wa Kampuni ya JETRO, Hiroyuki
Ishige, baada ya mazungumzo yao wakati Makamu Dkt Bilal, akiwa katika
ziara yake nchini Japan, leo.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika mazungumzo na Rais wa JAICA, Akihiko Tanaka, yaliyofanyika
wakati walipokutana kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake nchini Japan,
leo Mei 20, 2014. Kulia ni Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe
(wa pili kulia) ni Balozi wa Tanzania nchini Japan, Salome Sijaona.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika mazungumzo na Rais wa JAICA, Akihiko Tanaka, yaliyofanyika
wakati walipokutana kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake nchini Japan,
leo.
Na Sufianimafoto Reporter, Japan
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanza leo ziara ya Kikazi
nchini Japan, ziara inayolenga kuongeza ushirikiano baina ya Japan na
Tanzania ikizingatia maeneo ya uwekezaji na ubadilishaji wa teknolojia
baina ya nchi hizi mbili. Mheshimiwa Makamu wa Rais baada ya kuwasili
nchini hapa na kukutana na viongozi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Japan
ulio chini ya Balozi Salome Sijaona, alianza ziara hiyo kwa kutembelea
Ofisi ya Wizara ya Biashara Uchumi na Viwanda na kukutana na Waziri wa
Wizara hiyo Mheshimiwa, Toshimitsu Motegi, ambaye alimfahamisha
Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu maeneo ambayo Japan imekuwa
ikishirikiana na Tanzania, sambamba na yale ambayo ingetarajia
kushirikiana zaidi katika siku zijazo.
Akiwa
wizarani hapo Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata taarifa kuhusu makampuni
ya Japan ambayo yana nia ya kuwekeza Tanzania na kuelezwa namna
yalivyojipanga kushirikiana na Tanzania kutimiza azma zao za uwekezaji
na pia akatumia nafasi hiyo kuwaeleza kuwa Tanzania inashukuru kuona
Japan ikitangaza fursa za uwekezaji nchini Tanzania.
Pia
aliufahamisha uongozi wa wizara hiyo kuwa kwa sasa kuna ushindani mkubwa
wa kiuwekezaji nchini Tanzania hasa katika sekta za mafuta na gesi na
hivyo kazi ya Tanzania ni kutazama fursa ambazo zitakidhi matakwa ya
Wananchi wake na kutoa nafasi kwa makampuni ya kigeni yanayotambua na
kuthamini sera za uwekezaji zilizopo nchini huku yakiwa radhi kuchangia
katika kupunguza umaskini nchini badala ya kutafuta faida peke yake.
"Nafahamu
kampuni kutoka Japan zina nia njema ya kustusaidia kukabiliana na
umaskini wa wananchi wetu, tunashukuru sana kwa moyo huo na karibuni
kuwekeza Tanzania," alisema.
Baada ya
kikao hicho Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata fursa ya kufanya
mazungumzo na Mwenyekiti wa JETRO, Hiroyuki Ishige, ambaye aliongozana
na baadhi ya viongozi wa kampuni hi yo na kuzungumzia nia ya Japan
kutanua uwekezaji wa makampuni yao nje ya Japan, sambamba na Makampuni
ya Nje kuwekeza Japan.
Uongozi
wa JETRO ulieleza nia yake ya kufungua ofisi ya kuhamasisha uwekezaji
nchini Tanzania na ukafafanua kuwa mazungumzo ya kufikia lengo hilo
yanaenda vizuri huku wakimtaka Mheshimiwa Makamu wa Rais kuendelea
kuwasaidia ili wafanikishe azma hiyo. Balozi wa Japan nchini Tanzania,
Masaki Okada, alifafanua kuwa ujio wa JETRO nchini Tanzania utafungua
ukurasa mpya katika uwekezaji na pia utasaidia nchi hizi mbili kudumisha
uhusiano wake ambao sasa unaakisi katika masuala ya teknolojia na
uchumi.
Sambamba
na hilo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata nafasi ya kukutana na Ujumbe
kutoka JICA, ulioongozwa na Rais wake, Akihiko Tanaka, ambao uliishukuru
serikali ya Tanzania kukubaliana na miradi mbalimbali wanayoitekeleza
nchini Tanzania huku akisisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano baina ya
nchi hizi mbili ili wananchi wa nchi zote wazidi kunufaika.
Kwa
upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye katika ziara hii
ameambatana na Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe alifafanua
kuwa, Tanzania inathamini uhusiano wake na Japan sambamba na mchango
wake katika sekta mbalimbali na kwamba Tanzania ina tamaa kubwa ya kuona
urekebishaji wa miundombinu yake hasa Reli ya Kati maeneo ambayo
yamekabidhiwa kwa Japan yanafanyiwa kazi kwa wakati ili kukuza uchumi wa
Tanzania na nchi jirani zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam katika
kupitisha mizigo yake.








