DK. SHEN ATEMBELEA BANDARI YA ZANZIBAR
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/dk-shen-atembelea-bandari-ya-zanzibar.html
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Muhamed Shein
akifuatana na viongozi wa Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano
wakiingia lango kuu la Bandari ya Zanzibar iliyop Mlindi alipotembelea
bandari hiyo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Muhamed Shein
akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Affan
Othman Maalim (alievaa suti bluu na kofia) baada ya kutembelea ghala
lililokuwa likitumika kuhifadhia pembejeo za kilimo alipotembelea
bandari hiyo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Ali Muhamed Shein
akifuatana na viongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar kuangalia
utendaji wa kazi katika bandari hiyo ambayo hivi sasa meli kubwa ya
makontena zinafunga gati na kushusha mizigo kwa wepesi.
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20 Mei , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali
imelitaka Shirika la Bandari kuchukua hatua za haraka kushughulikia
tatizo la msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi ili shughuli
za bandari hiyo ziweze kufanyika kwa ufanisi.
Akizungumza
mara baada ya kutembelea bandari hiyo pamoja na eneo linalohifadhia
makontena matupu karibu na hoteli ya Bwawani wilaya ya mjini Unguja,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein alisema kwa ujumla hali hairidhishi katika bandari hiyo kutokana
na msongomano wa makontena.
“Bandari
haina nafasi ya kuweka makontena yote yanayoingia na yanayotoka. Hali
hainiridhishi mimi na kila mtu hapa. Kwa mfano leo hii bandarini kuna
meli inashusha makontena karibu 350 mengine yakijazana kila mahala mpaka
hapa Bwawani” Dk. Shein alifafanua.
Alijibu
swali kuhusu madhumuni ya ziara hiyo alisema ilikuwa ni kuona maeneo
yote ya bandari yakiwemo ya kuwekea makontena na pamoja na maghala
mbalimbali ili kuona kipi kinaweza kufanyika kupata eneo kwa ajili ya
kuondoa tatizo la msongomano wa makontena katika bandari hiyo.
Aliukumbusha
uongozi wa Shirika hilo kuwa sehemu ya kuwekea makontena la Bwawani ni
ya muda tu kama ilivyokubaliwa wakati wa uongozi uliopita wa Shirika
hilo ulipokabidhiwa eneo hilo hivyo ana hakikika kuwa tangu wakati huo
walikuwa wanafanya mipango mbadala wa kupata eneo jingine.
Alifafanua
kuwa eneo hilo limo katika mpango wa Serikali wa uwekezaji kwa shughuli
nyingine za maendeleo ambapo wakati wo wote linaweza kuchukuliwa kwa
shughuli hizo hivyo uongozi wa bandari hauna budi kuzingatia hilo kwa
kuharakisha mipango yake ya kuondoka katika eneo hilo.
Hata
hivyo Dk. Shein alikiri kuwa Bandari ya Malindi hivi sasa imeshakuwa
ndogo na itakuwa vigumu kukidhi mahitaji ya matumizi ya sasa ya bandari
hasa baada ya mfumo wa usafirishaji wa bidhaa kubadilika kuwa wa kutumia
makontena.
Kwa
hiyo alieleza kuwa ndio maana jitihada za Serikali zimeelekezwa katika
kutekeleza mpango wake wa ujenzi wa bandari mpya na ya kisasa huko
katika eneo la Mpigaduru liliko kilomita chache kutoka bandari ya sasa
ya Malindi.
Katika
ziara hiyo Dk. Shein amelitaka Shirika hilo kuangalia upya matumizi
bora ya baadhi ya majengo yake kwa kuyajenga upya ili kupata ofisi za
kisasa na bora ili Shirika liweze kutoa huduma vizuri kwa wateja wake.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Bwana Abdalla Juma
Abdalla alisema lengo la kuhifadhi makontena matupu katika eneo la
Bwawani ni kutoa nafasi kwa makontena yenye bidhaa kuweza kushushwa
kutoka melini na kuokoa gharama na usumbufu pindi makontena hayo
yakichelewa kushushwa kutoka melini.
Alibainisha
kuwa Shirika lake inalipa kipaumbele suala la kuondosha msongomano wa
makontena bandarini hapo na kwamba uongozi wa bandari wakati wote
umekuwa ukihakikisha kunakuwepo na ufanisi katika utendaji wake.
Katika
ziara hiyo Dk. Shein alifuatana na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya
Miundombinu na Mawasiliano, Wizara ya Kilimo na Maliasili pamoja na
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Maalim Abdalla Mwinyi Khamis.